*Awahimiza kuzingatia afya zao kuepuka magonjwa, changamoto ya afya ya akili
*Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewataka watendaji na watumishi wa Wizara ya Madini kuzingatia uadilifu na maadali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuhakikisha Sekta ya Madini inakua na kuendelea kuongeza tija ikiwa ni pamoja na kuendelea kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa (GDP) na maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo Machi 18, 2025 wakati akifungua Kikao kazi cha Watumishi wa Wizara ya Madini kilichofanyika Jijini Dodoma ambapo amewataka watendaji na watumishi hao kuzingatia miongozo ya Serikali sambamba na kuepuka vitendo visivyo vya kimaadili kama kupokea rushwa.
“Rushwa ni adui mkubwa wa haki, rushwa inaingia katika makosa ya kimaadili na uadilifu, lengo letu sisi ni kutoa huduma bora kwa wateja wetu, kama Wizara, tunataka kuwa mfano bora wa utumishi wa umma” amesema Mbibo.
Katika hatua nyingine, Mbibo amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kuzingatia masuala muhimu ya kiafya ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya mwili ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama shinikizo la damu, kisukari, maradhi ya moyo, afya ya akili na mengineyo sambamba na magonjwa ya kuambukizwa kama UKIMWI.
Pia, Mbibo ametumia nafasi hiyo kutoa pole kwa watumishi wa Wizara kufutia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Tehama Edson Nkongo aliyefariki Machi 12, 2025 na kuwataka kuendelea kumuasisi mtumishi huyo kwa kufanya kazi kwa ubunifu na kujitolea katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Madini Festus Mbwilo amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho cha watumishi wa Wizara ni kuhakikisha ufanisi unaongezeka katika utekelezaji wa programu na majukumu ya Wizara ili kufikia malengo ya Wizara na Serikali kwa ujumla kupitia Sekta ya Madini.