Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Mavere Tukai akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17,2025 katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Bohari ya Dawa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Mavere Tukai akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17,2025 katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Bohari ya Dawa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeanza ujenzi wa maghala mapya toka mwezi Agosti 2023 katika Kanda ya Mtwara na Dodoma ili kukidhi upungufu uliojitokeza.
Hayo yamesemwa leo Machi 19,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Mavere Tukai,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Bohari ya Dawa katika kipindi cha miaka minne chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa ujenzi huu unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi 2025 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 42. Fedha zinazotumika katika ujenzi wa maghala zimetolewa na
Serikali.
“Ghala linalojengwa Mtwara lina ukubwa wa mita za mraba 4,800 na lile lililopo Dodoma lina ukubwa wa mita za mraba 7200, hivyo kufanya ongezeko la uhifadhi kutoka mita za mraba 56,858.57 na kufikia mita za mraba 68,858.57. Miradi hii imekamilika kwa wastani wa asilimia 96.”amesema Bw.Mavere
Aidha ameelezea kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuendana na ukuaji wa idadi ya watu na ongezeko la uwekezaji unaofanywa na Serikali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, kupunguza gharama za uhifadhi na kuimarisha utunzaji wa bidhaa za afya kwa kuhakikisha bidhaa za afya zinahifadhiwa kwenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya utunzaji salama wa bidhaa za afya na vituo vya kutolea huduma za afya zinapata bidhaa husika kwa wakati.
Bw.Mavere amesema kuwa Ghala kuu la Dodoma litahudumia Kanda za Dodoma, Mwanza, Kagera, Iringa, Mbeya na Tabora kwa lengo la kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana za kutosha kwenye Kanda hizo na kwa wakati na kupunguza muda uliokuwa unapotea kufuata bidhaa za afya kutoka Dar es salaam.
Pia, kukamilika kwa ghala hilo kutapunguza gharama za uendeshaji wa taasisi kwakua kanda hizo hazitafuata mizigo ghala kuu la Dar es Salaam, bali zitachukua mizigo yao kutoka ghala kuu la Dodoma hivyo kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana muda mwingi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Hata hivyo amesema katika kuendeleza uwekezaji huu, Serikali ya awamu ya sita imeweza kutoa kiasi cha shilingi bilioni 16.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa ghala la kuhifadhi bidhaa za afya katika kanda ya Mwanza na shilingi bilioni 3.8 kwa kuwezesha kuanzisha ujenzi wa ghala la Chato mkoani Geita.
Akizungumza upatikanaji wa bidhaa za afya amesema Bohari ya Dawa imeendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Uwepo wa bidhaa za afya umekuwa ukipimwa kwa bidhaa za afya ashiria 290 lakini kutokana na kuimarishwa mifumo ya utoaji huduma na nia ya Serikali kuboresha maisha ya Watanzania kuanzia mwaka wa fedha 2023/24, idadi ya bidhaa ashiria zinazotumika kupima hali ya upimaji wa bidhaa za afya zimeongezeka kutoka bidhaa 290 hadi kufikia bidhaa 382,
Hali ya uwepo wa bidhaa za afya ashiria 382 imeongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 2021/2022 hadi asilimia 67 mwezi Februari, 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 23,Kwa ujuma hali ya upatikani wa bidhaa za afya umekuwa ukiimarika mwaka hadi
mwaka,”amesema
Amesema upatikanaji wa bidhaa za Afya ni mafanikio makubwa ambapo kabla ya 2021/2022 ,MSD ilipimwa kwa bidhaa chache zaidi lakini sasa wanapimwa kwa bidhaa 382.
“Wakati tunaanza 2021/22, asilimia kama 42 tu ndiyo ilikuwa inapatikana kwa zile bidhaa ashiria 382 lakini mpaka February mwaka huu tulikuwa tumeshafima asilimia 67 na mpaka tufikie Juni 30 kwamba huu tutakuwa tunaelekea asilimia 90,”amesema
MSD)ni ni taasisi inayomilikiwa na Serikali iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Sheria ya Bohari ya Dawa Na.13 ikiwa na majukumu manne (4), Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na vile vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Katika kipindi cha awamu ya sita ya uongozi, Vituo vya kutolea huduma za afya vinavyohudumiwa na MSD vimeongezeka na kufikia vituo 8,466 mwaka 2024/2025 kutoka vituo 7,095 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la vituo 1,371 ambapo ni ongezeko la asilimia 19.
Ongezeko kubwa la vituo vya kutolea huduma za afya vinavyopelekewa bidhaa na MSD lilikuwa kwenye zahanati ambapo vituo 1,102 viliongezeka na ndipo ambapo wananchi wengi wanapata huduma, Bohari ya Dawa imeendelea kuhudumia vituo hivi kupitia Kanda zake 10 zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.