Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2025. Hafla hiyo itafanyika siku ya Jumapili, tarehe 13 Aprili 2025, katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema kuwa maandalizi ya hafla hiyo yamekamilika na kwamba ni heshima kubwa kwa sekta ya elimu kuwa na ugeni huo wa juu unaoonyesha namna ambavyo serikali inatambua mchango wa uandishi bunifu katika kukuza lugha ya Kiswahili, maarifa, na utamaduni wa taifa.
Profesa Mkenda alisema kuwa Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni miongoni mwa njia bora za kuenzi fikra, falsafa na maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliweka msingi wa matumizi na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya elimu, umoja na maendeleo ya jamii ya Watanzania.
“Tuzo hii ni heshima kwa Mwalimu Nyerere lakini pia ni jukwaa mahsusi kwa waandishi chipukizi na wakongwe kuonyesha umahiri wao katika nyanja mbalimbali za uandishi kama vile riwaya, ushairi, hadithi za watoto na tamthiliya,” alisema Prof. Mkenda.
Aidha, Waziri alieleza kuwa katika hafla hiyo, washindi wa Tuzo kwa kila kundi watatangazwa rasmi, na zawadi zitakazotolewa zitajumuisha fedha taslimu, vyeti na kuchapishwa kwa kazi za washindi wa kwanza ambazo zitasambazwa katika shule na maktaba mbalimbali nchini kupitia ushirikiano na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Profesa Penina Mlama alisisitiza kuwa majaji wamekamilisha kazi ya kusoma miswada iliyowasilishwa na tayari orodha teule ya waandishi waliopendekezwa imechapishwa. Alieleza kuwa washindi wa mwisho watachaguliwa kutoka kwenye orodha hiyo teule.
Profesa Mlama alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha Watanzania wote kuhudhuria hafla hiyo ya kihistoria, huku akitoa shukrani kwa waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kuutangazia umma juu ya umuhimu wa Tuzo hii tangu kuanzishwa kwake mwaka wa fedha 2022/23.