*Utoshekevu huo umetokana na ongezeko la matumizi ya mbolea ya ruzuku
*Mbolea ya ruzuku ya Sh Bilioni 131 ilisambazwa kwa wakulima katika mwaka 2024/2025
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema nchi imeendelea kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128, utoshelevu huo unatokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani milioni 20.4 katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 hadi tani milioni 22.8 msimu wa mwaka 2023/2024.
Pia, Waziri Mkuu amesema ongezeko hilo limetokana na ongezeko la matumizi ya mbolea iliyotolewa kwa wakulima kupitia mpango wa ruzuku, kuongezeka kwa mtandao wa kilimo cha umwagiliaji, kuimarika kwa huduma za ugani na matumizi ya mbegu bora.
Ameyasema hayo jana (Jumatano, Aprili 9, 2025) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Mtumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma.
Alisema licha ya kuliwezesha Taifa kujitosheleza kwa chakula, sekta ya kilimo ni muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kutokana na mchango wake katika uzalishaji wa ajira, biashara na malighafi za viwandani.
Kutokana na umuhimu huo, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mahsusi za kuendeleza sekta hii muhimu kwa uchumi wa Taifa letu. Moja ya hatua hizo ni utekelezaji wa Programu ya kuendeleza sekta ya kilimo (ASDP).
“Tayari Serikali imekamilisha mapitio na uhuishaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II) kwa muhula wa mwisho utakaokamilika mwaka 2030. Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa programu hiyo na mikakati inayolenga kuitekeleza ili kuimarisha sekta ya kilimo.”
Waziri Mkuu alisema sambamba na utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kuendeleza kilimo, ambayo ni pamoja na kutoa mbegu na pembejeo za kilimo, kutoa mikopo ya kilimo kwa wananchi, kuanzisha skimu za umwagiliaji na kuimarisha ushirika.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema hali ya upatikanaji wa mbolea nchini imeendelea kuimarika ambapo hadi tarehe 31 Januari, 2025 kulikuwa na jumla ya tani milioni 1.21 sawa na asilimia 80.9 ya makisio ya mahitaji ya tani milioni 1.5 za mbolea kwa msimu wa mwaka 2024/2025.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa alisema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, tani 388,619.87 za mbolea yenye ruzuku ya thamani shilingi bilioni 131.66 imesambazwa kwa wakulima 4,223,278.