
Wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi katika mwalo wa Mnyara, Kata ya Nkome, Wilaya ya Geita, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia mkopo wa shilingi milioni 117 uliowasaidia kuboresha shughuli za ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Wakizungumza wakati wa zoezi la uvunaji wa samaki katika vizimba walivyowezeshwa kupitia mkopo huo, wananchi hao wamesema mradi huo umechangia kuongeza kipato, kuinua hali ya maisha yao, na kupunguza utegemezi wa uvuvi wa asili ambao mara kadhaa huambatana na vitendo vya uvuvi haramu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Karia Rajabu, alieleza kuridhishwa na juhudi za kikundi hicho na kuahidi kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana nao kwa kuwawezesha kupata mikopo zaidi ili kukuza shughuli zao.
Naye Afisa Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Paul Emmanuel, alisema kuwa ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba ni mbinu rafiki kwa mazingira na yenye tija kubwa, kwani imechangia kuongezeka kwa upatikanaji wa samaki kwa wingi tofauti na uvuvi wa kienyeji.
Serikali kupitia halmashauri inaendelea kuhimiza wavuvi kutumia mbinu bora na endelevu za uzalishaji ili kuhakikisha rasilimali za maji zinatumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.