Na Fauzia Mussa
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama wakati wote wa mashindano ya Samia na Mwinyi Cup, yanayoendelea kufanyika katika mkoa huo, ili kuhakikisha vijana wanashiriki katika mazingira salama na tulivu.
Akizungumza na ujumbe kutoka Taasisi ya Twende na Mama Sports Promotion, waandaaji wa mashindano hayo, waliofika ofisini kwake kujitambulisha kabla ya uzinduzi rasmi, Mkuu huyo wa Mkoa aliwapongeza kwa kuja na wazo hilo, akieleza kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi za viongozi wa kitaifa katika kukuza sekta ya michezo na kuwaunganisha vijana kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
“Kuimarisha ulinzi ni jukumu la msingi kwa Serikali ili kuhakikisha vijana wetu wanashiriki michezo bila hofu yoyote,” alisema Mustafa na kuongeza kuwa Mkoa wa Mjini Magharibi unajivunia kuwa wa kwanza kuendesha mashindano hayo.
Kuhusu kutofanyika kwa michezo hiyo katika Uwanja wa Mao Zedong, alisema kuwa uwanja huo umehifadhiwa kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya CHAN na AFCON. Alisisitiza kuwa hatua hiyo si kwa nia mbaya, bali ni sehemu ya kulinda maslahi ya taifa kwa kutunza viwanja hivyo kutokana na gharama kubwa za uendeshaji na matengenezo.
Kwa upande wake, Haji Mohammed Haji, Mkurugenzi Mtendaji wa Twende na Mama Sports Promotion, alisema taasisi hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuunga mkono jitihada za viongozi wa kitaifa kwa kutangaza mambo mazuri wanayoyafanya, sambamba na kuhamasisha vijana kushiriki michezo ili kuwaepusha na makundi hatarishi.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa taasisi hiyo uliambatana na bondia maarufu Karim Mandonga pamoja na msanii wa vichekesho Mau Fundi. Walifanya matembezi ya kuhamasisha wananchi katika mitaa ya Jang’ombe na Mboriborini, kabla ya mchezo wa Ngao ya Hisani uliochezwa kama sehemu ya uzinduzi rasmi wa mashindano hayo yanayoshirikisha jumla ya timu 32.
“Mashindano haya yatahusisha timu 32, na Mkoa wa Mjini Magharibi unakuwa wa kwanza kuyaendesha,” alieleza Haji.
Bondia Karim Mandonga aliipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuwajali wananchi, huku Mau Fundi akitoa pongezi kwa wakazi wa Zanzibar kwa mapokezi mazuri, akieleza kuwa visiwa hivyo ni sehemu tulivu yenye watu wakarimu.
Mashindano ya Samia na Mwinyi Cup yanaendelea kushika kasi, yakishirikisha timu kutoka mikoa mbalimbali nchini, yakiwa na lengo la kuimarisha mshikamano, amani na maendeleo ya michezo miongoni mwa vijana wa Tanzania.