Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijibu maswali ya papo kwa pao ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma Aprili 24, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
….
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea na mpango wa kuyaendeleza mabonde nchini kwa kuyatumia kutoa huduma za kijamii ikiwemo upatikanaji wa maji na nishati ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na mafuriko.
Amesema moja ya mkakati uliochukuliwa na Serikali ni kuunda mamlaka za mabonde zenye wajibu wa kufanya ufuatiliaji wa mwenendo upitishaji maji na kuratibu namna nzuri ya utumiaji wa mabonde hayo.
Amesema hayo leo (Alhamisi, Aprili 24, 2025) wakati akijibu swali la mbunge wa Kyela, Ally Anyigugile Jumbe aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kukabiliana na mafuriko nchini, wakati wa kipindi cha Maswali ya Wabunge kwa Waziri Mkuu.
“Kama ambavyo tumeona kwenye bonde la mto Rufiji, tumeamua kuanzisha mradi mkubwa sana wa kuzalisha umeme. Nilifanya ziara mkoani Morogoro ambapo tunachimba bwawa kubwa ambalo linategemea maji ya mto Ruvu; ujenzi wa mabwawa haya yataleta maslahi kwa Watanzania ikiwemo kwenye sekta za kilimo, nishati, maji na mifugo.”
Ameongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha inaongeza bajeti kwenye Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). “Tunataka kuhakikisha maji yanayosababishwa na mvua hayapotei bure bali tunayatumia kwa faida ya Watanzania.”
Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kusimamia maslahi ya watumishi, mishahara na madai mbalimbali ili kuhakikisha yanalipwa kwa wakati na waweze kuendesha maisha yao.
Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Jacob Tarimo aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wafanyakazi wa kada na elimu zinazofanana wanapata mshahara unaofanana.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeanzisha idara ambayo inashughulikia mishahara, posho na marupurupu inayofanya mapitio kila mwaka na kuona mabadiliko ya kiuchumi ya nchi kama yanakwenda sambamba na pato ambalo linamuwezesha mtumishi wa umma kutekeleza majukumu yake.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mikakati ya Serikali wa kukabiliana na ukatili kwenye jamii, Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza mipango mbalimbali ya kudhibiti masuala ya ukatili ikiwemo kutoa elimu pamoja na kushirikiana na wadau na taasisi zinazopinga ukatili.
Ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la Stella Simon Fiyao (Viti Maalum) aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuandaa vitengo maalum shuleni, vyuoni, ngazi za jamii na kwenye ofisi ili kusaidia kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Mheshimiwa Majaliwa aliongeza kuwa katika kuhakikikisha nchi inakuwa salama dhidi ya ukatili kwenye jamii, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda wizara maalum inayosimamia masuala ya kijamii pamoja na kuhakikisha inakabiliana na ukatili kwenye jamii.
“Wizara hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweka mifumo ya kisheria inayomlinda kila mmoja dhidi ya ukatili wa aina yoyote ile. Tumeandaa madawati ya jinsia kwenye taasisi zote za umma ikiwemo shuleni, vyuoni pamoja na kwenye taasisi zinazotoa huduma za kiulinzi kama Jeshi la Polisi na Magereza.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema pamoja na jitihada hizo, kila Mtanzania anapaswa kuwa mlinzi dhidi ya ukatili kwenye jamii. “Matukio haya ambayo yanajitokeza katika jamii, yanaondoa haki ya msingi ya kibinadamu pale anapotendewa ukatili dhidi yake na hivyo kila mmoja awe mlinzi wa matendo haya popote pale.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijibu maswali ya papo kwa pao ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma Aprili 24, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)