Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, akitembelea mabanda na kujionea kazi za TEHAMA zilizobuniwa na wasichana wakati wa Maadhimisho ya siku ys Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Aprili 24.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Maadhimisho ya siku ys Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Aprili 24.
Na Mwandishi wetu.
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, ametoa wito kwa walimu nchini kuanzisha vilabu vya kidijitali katika shule kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu, ili kuhamasisha vijana hasa wasichana kupata ujuzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza jijini Dar es Salaam Aprili 25, 2025 katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA, Waziri Silaa alisema vilabu hivyo vitakuwa chachu ya kuibua vipaji na kusaidia jamii kupata suluhisho la changamoto mbalimbali kwa kutumia teknolojia.
“Serikali imekuwa ikiendeleza jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi wake wanapata ujuzi wa kutumia teknolojia za kidijitali zinazoweza kuwawezesha kiuchumi na kijamii,” alisema Silaa.
Aidha, alieleza kuwa mitaala ya elimu imeboreshwa ili kuendana na mabadiliko ya kasi ya teknolojia, na kumwezesha mwanafunzi kupata ujuzi wa kutumia TEHAMA katika ubunifu wa suluhisho za matatizo ya kijamii.
“Mitaala mipya inalenga kumsaidia kijana hasa msichana kufikia ndoto zake kupitia elimu ya TEHAMA,” aliongeza Waziri.
Pia alisisitiza kuwa serikali ina mipango madhubuti ya kuhakikisha taifa linanufaika na uchumi wa kidijitali, ikiwemo kuboresha miundombinu ya mawasiliano yenye kasi kubwa ili kuhakikisha teknolojia inawafikia wananchi wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Bakari, alisema maadhimisho hayo yamekusudiwa kuhamasisha ubunifu na matumizi ya TEHAMA kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
“Tuna vilabu vya kidijitali hata kwenye shule za msingi, lengo ni kukuza uelewa wa TEHAMA, kuibua miradi ya ubunifu na kusaidia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi,” alisema Dkt. Bakari.
Aliongeza kuwa kupitia vilabu hivyo, wanafunzi watapata msukumo wa kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) na hatimaye kufanikisha ndoto zao.