Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Slaa, akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam Aprili 28, 2025.
Mtendaji Mkuu wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, akizungumza wakati akielezea namna Airtel Tanzania ilivyojipanga kukabiliana na utapeli wa mitandaoni kupitia akili mnemba.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel Tanzania Beatrice Singano akifafanua baadhi ya mambo katika hafla hiyo ya uzinduzi.
………………
Katika hatua ya kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya utapeli kupitia simu za mkononi, Kampuni ya Airtel Tanzania imezindua programu mpya inayotumia teknolojia ya Akili Mnemba, ikiwa ni kampuni ya kwanza nchini kuanzisha mpango wa aina hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Slaa, alisema uzinduzi wa programu hiyo unaonyesha mshikamano wa sekta binafsi katika kusaidia juhudi za Serikali za kupambana na utapeli wa mtandaoni.
“Serikali inaendelea kuhimiza wabunifu na wadau wa mawasiliano kutumia teknolojia za kisasa kama Akili Mnemba katika kuzuia matukio ya utapeli,” alisema Waziri Slaa. Aidha, aliwatahadharisha wananchi kuwa na tahadhari na kutotoa taarifa zao binafsi kwa watu wasiowafahamu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya vitendo vya kihalifu mtandaoni.
“Tunajivunia kuwa kampuni ya kwanza nchini kuzindua programu ya aina hii na tutaendeleza jitihada zetu kuhakikisha usalama wa mawasiliano ya wateja wetu,” alisema Kamoto.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Udhibiti wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, aliwahimiza waandishi wa habari kuwa mabalozi wa kampeni hiyo kwa kuhakikisha ujumbe wa tahadhari unawafikia wananchi. Alikumbusha kuwa namba rasmi ya huduma kwa wateja ya Airtel ni 100 pekee.
Programu ya Akili Mnemba inalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa visa vya utapeli kupitia simu za mkononi, huku ikilenga kulinda taarifa binafsi za watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini.