Serikali, itaendelea kuimarisha maendeleo katika ya habari, vijana, utamaduni na michezo ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Tabia Maulid Mwita, amesema hayo wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi huko Rahaleo Wilaya ya Mjini.
Amesema, mafanikio yanayopatikana hadi sasa ni matokeo ya utekelezaji wa programu za Maendeleo ikiwemo sekta ta Habari, Vijana, utamaduni, Michezo pamoja na Uendeshaji na Mipango.
Aidha amesema kuwa, Bajeti hiyo ni muelekeo mzuri wa kuendeleza sekta ya michezo, kupitia ujenzi wa viwanja mbalimbali unaoendelea nchini.
Hata hivyo, ameishukuru Kamati hiyo kwa kutoa ushauri wa mara kwa mara kwa Wizara ya habari Vijana, Utamaduni na Michezo jambo ambao limesaidia kuboresha utendaji na kuahidi kuyazingatia mapendekezo yote yaliotolewa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Ustawi wa jamii ya Baraza la Wawakilishi Mhe. Sabiha Filfil Thani amesema kamati hiyo, itaendelea kusiimamia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi na kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuwaletea maendeleo Wananchi.
Aidha ameipongeza Wizara hiyo kwa juhudi kubwa inayozichukuwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Viwanja vya Michezo.
Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Bihindi Hamad Khamis amesema bajeti hiyo ni nzuri na kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango kuwapatia mgao ili waweze kutekeleza miradi walioianzisha.
Nae Mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Bahati Khamis Kombo, amesema Bajeti hiyo imejaa matumaini kwani wakati itakapotekelezwa itaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo na kutoa faida kwa Wananchi ikiwemo Vijana.
Makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti ya Wizara ya habari, Vijana, utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, inatarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachotarajiwa kuanza hivi karibuni.