Na Sophia Kingimali.
MKUU wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta – Furahika, Dkt David Msuya ametoa wito kwa waajiriwa wa Serikali na binafsi kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya masomo ya jioni yanayoanza Mei 5, mwaka huu huku wakianzisha kozi mpya ya biashara.
Amesema masomo hayo yatawasaidia wafanyakazi hao kuendana na mahitaji ya soko la ajira ya sasa na kuachana na kufanyakazi kwa mazoea bila kuangalia mabadiliko ya sanyansi na teknoloji.
Dkt Msuya ameyasema hayo leo Aprili 30,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kufafanua kwamba masomo yataanza saa 11 jioni hadi saa 1:00 usiku na yatachukua miezi mitatu hadi mwaka mmoja kulingana na kozi.
Amesema kozi hizo zitawaongeze maarifa katika utendaji kazi wao na kuleta tija kwa Serikali, taasisi na taifa kwa ujumla, hivyo ni kundi hilo likajitokeza kwa wingi kusoma masomo hayo ya jioni kwa kozi mbalimbali.
Ameongeza kuwa waajiriwa watakaofika chuoni hapo kusoma masomo hayo wataigharamia vifaa ‘stationery’ pekee, jambo ambayo ni dhahiri linatoa nafasi kwa kundi kubwa kujitokeza kusoma kwani ni sawa na bure.
Dkt Msuya amezitaja kozi zitakazofundishwa chuoni hapo kwa muda wa jioni kuwa ni Public Administration (Utawala wa Umma), Human Resource Management (HRM), Leadership and Management pamoja na Project Planning and Management, ambapo kozi zote hizi zitatolewa kwa mwaka mmoja .
Kozi nyengine ni za Fedha na Manunuzi ambapo zinatolewa kwa wiki mbili hadi 12 ambayo ni ‘Ethics and Integrity in Public service’ itakayotolewa kwa miezi 3, pia itatolewa kozi ya biashara itakayogawanywa katika makundi manne ambayo ni Marketing and Sales, Accounting and Finance, Business administration with Human resources.
Aidha, amesema kuwa chuo hicho, kinatoa fursa sawa kwa watanzania katika kuwaendeleza vipaji vyao na kutoa ujuzi ili waweze kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Chuo hicho ambacho kipo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam kimesajiliwa na NACTVET kwa namba REG/NACTVET/1113 kinatoa kozi mbalimbali ikiwemo hoteli, ushonaji, Ufundi magari, ualimu, ambapo kozi zote hizo hutolewa bure kwa vijana waliomaliza darasa la Saba, kidato cha nne na wale waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali za maisha