Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ni bajeti ya haki inayolenga kuwapatia Watanzania, hususani wanyonge, fursa sawa ya kupata haki katika kila kona ya nchi.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo, Dkt. Ndumbaro amesema bajeti hiyo inaenda kufuta machozi ya Watanzania waliodhulumiwa haki kwa muda mrefu.
“Bajeti hii sisi tunaita bajeti ya haki. Bajeti ambayo inaenda kumpa haki Mtanzania, kutoa shibe kwa Watanzania wenye njaa na kiu ya haki. Italeta mwanga na kuondoa giza la dhulma ya haki kwa Watanzania wanyonge katika kona zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Waziri huyo ameeleza kuwa bajeti hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa haki, hasa kwa wananchi wa kawaida ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali katika kupata huduma za kisheria.