Mkuu wa Chuo cha Kodi Tanzania (ITA), Profesa Isaya Jairo akizungumza na waandishi wa habari Mei 2, 2025 jijini Dar es Salaam, kuhusu kongamano la kwanza la kodi litakalofanyika Mei 8, 2025 katika hoteli ya Johari Rotana, ambalo litawaleta pamoja wadau kujadili mikakati ya kupanua wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji wa hiari .
……
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo cha Kodi Tanzania (ITA) kimeandaa kongamano la kwanza la kodi litakalowaleta pamoja watunga sera, wataalamu wa kodi, wafanyabiashara, watafiti kujadili mikakati ya kupanua wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji kwa hiari kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.
Kongamano hilo litafanyika Mei 8, 2025 katika hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, likiwa mada kuu isemayo :‘Kuongeza wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji kodi kwa hiari Tanzania’, huku mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha Mhe. Lameck Mwigulu Nchemba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2, 2025 jijini Dar es Salaam Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Profesa Isaya Jairo, amesema kuwa washiriki wa kongamano hilo watapata nafasi ya kuchambua mada muhimu ikiwemo kupanua wigo wa kodi na kurasimisha sekta isiyo rasmi.
Profesa Jairo amesema kuwa washiriki watajikita zaidi kujadili uimarishwaji wa ulipaji wa kodi kwa hiari na kuongeza wigo wa kodi, mtazamo wa sekta binafsi na wafanyabiashara pamoja na kuweka mikakati ya uarasimishaji na motisha kwa walipa kodi kwa hiari.
“Mada nyengine ni kuzuia ukwepaji wa kodi ambapo washiriki watajikita zaidi katika mikakati ya kuzuia ukwepaji wa kodi, njia, sheria na kanuni. Pia watajadili mikakati ya utupwaji wa bidhaa hafifu kutoka nje ya nchi na kuongeza uhiari wa ulipaji kodi” amesema Profesa Jairo.
Amesema kuwa wanatarajia kongamano hilo litasaidia kuangalia mikakati ya kupanua wigo wa kodi, kupata utambuzi wa tabia katika kuongeza ulipaji wa kodi, kuchunguza njia ya kuongeza usawa wa kodi na kupunguza taratibu zisizo rasmi, kuimarisha ushirikiano kati ya wadau, kutegemeana na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa kodi pamoja na kutengeneza sera zinazotekelezeka.
“Nawakaribisha waalikwa wote kuhudhuria na kushiriki kikamilifu kongamano hili kwa pamoja tushirikiane kujadili na kupata njia bora ya kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari na kuongeza mapato ya nchi” amesema Profesa Jairo.