Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iguga Mkoani Tabora. Selwa Hamid akimkabidhi kitabu kichoelezea miradi ya maendeleo ya halmashauri hiyo, mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Igunga Lucas Bugota katika ukumbi wa halmashauri hiyo jana.
Na Lucas Raphael,Tabora
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iguga Mkoani Tabora. Selwa Hamid ameweka wazi matumizi ya fedha zilizotumika kwenye miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Afya, Elimu ya Msingi, Kilimo mifugo na uvuvi, Elimu ya sekondari, kwa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.
Akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani cha robo ya tatu kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora kilichohudhuriwa na madiwani, Mkuu wa Wilaya hiyo Sauda Mtondoo, Wakuu wa idara na baadhi ya wananchi wa Igunga.
Alisema jumla ya bilioni 41,405,035,302 zimetolewa na serikali inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika Wilaya Igunga.
Alisema katika sekta ya Afya vituo Vipya vya Afya Kata ya Itumba na Ziba kutoka vituo 4 hadi 6 zahanati mpya 9 na kufika jumla ya zahanati 73 majengo ya ICU, OPD, mionzi, Murtuary, wodi ya wanaume Shilingi Bilioni 1.1 na vifaa tiba thamani ya Tsh. Bilioni 1.5.
Sekta ya Elimu Msingi uwekezaji wa shilingi bilioni 5.8 katika kuimarisha miundombinu ya shule, ujenzi wa shule mpya 2, madarasa mapya 81 Tsh. Bilioni 2.38, ujenzi wa nyumba 4 za walimu (2 in 1) shilingi 200,000,000. ujenzi wa matundu ya vyoo 402 Tsh. 918,137,133 kukamilisha maboma ya madarasa 10 na nyumba 2 shilingi 175,000,000/=, fedha za ruzuku ya Elimu bila malipo shilingi 2,197,223,732.
Sekta ya Elimu Sekondari, shilingi 11,906,499,469/= zimejengwa shule 5 mpya ambapo ongezeko la madarasa 133 shilingi 2,580,000,000/= nyumba za walimu 12 zimeongezwa jumla ya shilingi 595,918,000/= matundu ya vyoo 171 yameongezeka shilingi 376, 200,006/= ukamilishaji wa maboma ya madarasa 24 nyumba 2, hostel 4, majengo ya utawala, mabwalo 2 na maktaba 3 Tsh. Bilioni 1.05.
Sekta ya kilimo mifugo na uvuvi shilingi 172 zimetumika katika ujenzi wa majosho 4 na nyumba mbili (2) za maafisa ugani, Aidha alisema mwezi mei 2025 Halmashauri ya wilaya ya Igunga imepokea Tsh. 790,000,000.00 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya shule, zahanati na vituo vya Afya. Pia shilingi 206,000,000.00 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya nyumba na vyoo katika shule za msingi.
Sambamba na hayo Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa kutokana na ushirikiano alioupata kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Madiwani ndiyo umewezesha Halmashauri kuwa na maendeleo mazuri kwa kusimamia kwa uadilifu fedha zinazotolewa na serikali pamoja na wanazokusanya kupitia mapato ya ndani.
Aidha mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kwa mwaka 2024/2025 makusanyo ya mapato ya ndani yamefikia asilimia 90.27% ambapo hadi sasa wamekusanya shilingi bilioni 4,868,633,690/= kati ya bilioni 5,393,316,000/= kwa malengo waliojiwekea.
Hata hivyo aliwahakikishia madiwani kuwa pamoja na wao kumaliza muda wao yeye na timu yake wataendelea kusimamia kwa ufanisi makusanyo ya fedha pamoja na matumizi ya fedha kwa mujibu wa sheria hadi watakapo jaliwa kurejea tena baada ya uchaguzi oktoba 2025.
Nae mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Igunga Lucas Bugota alimshukuru mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumpatia Mkurugenzi mchapakazi na mwenye kusimamia kwa uadilifu fedha za serikali sambamba na kuongeza mapato ya Halmashauri jambo ambalo ameipa heshima kubwa wilaya ya Igunga.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo aliwashukuru madiwani wote kwa ushirikiano waliouonyesha kwa kushirikiana katika kuijenga Halmashauri yao ambapo aliwaomba kwenda kufanya siasa za kistaarabu pasipo kuvunja sheria za nchi.
Nao baadhi ya madiwani Andrew Paulo wa Kata ya Kitangili, Emmanuel Cheyo wa Kata ya Ugaka na Eva Godfrey wa viti maalum Kata ya Ibologelo kwa nyakati tofauti walisema katika muda wote wa udiwani Mkurugenzi huyo amekuwa akiwapa ushirikiano wa kutosha na ndiyo maana Halmashauri imeendelea kupata hati safi.
“Kwa kweli huyu Mkurugenzi Selwa Hamid tunamshukuru sana amekuwa mstari wa mbele kutupa ushauri pia kupokea ushauri wetu na ndiyo maana mapato ya Igunga yapo juu na miradi yake imekuwa ikisimamiwa vizuri.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi Rehema Athumani, Aziza Iddi, Juma Salumu kwa nyakati tofauti walisema Mkurugenzi huyo amekuwa na mchango mzuri wa mahusiano kwa wananchi wa Igunga kwa kutatua kero nyingi zilizokuwepo na kuongeza kuwa wataendelea kumpa ushirikiano popote watakapo hitajika.