Mwamvua Mwinyi, Mafia
Mei 17,2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, ametoa rai kwa wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura ambao hawakuboresha taarifa zao katika awamu ya kwanza ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza kwa wingi katika awamu ya pili ili kupata uhalali wa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Aidha ametoa wito, kwa wananchi ambao ndugu au jamaa zao wamefariki dunia au wamepoteza sifa ya kupiga kura, kujitokeza kufuta taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Jaji Mwambegele alitoa wito huo, alipotembelea kituo cha Shule ya Msingi Ndagoni kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa zoezi hilo, ambalo linatarajiwa kufanyika kwa siku saba hadi Mei 22, 2025.
“Nimeshuhudia ufunguzi wa zoezi hili katika Shule ya Msingi Kilimahewa na kutembelea baadhi ya vituo vya jimbo hili.
“Nashukuru kuona zoezi linaendelea vizuri,ningependa kuwasihi watanzania kujitokeza kwa ajili ya kuboresha taarifa zao au kujiandikisha, “
“Usipojitokeza katika awamu hii ya pili, itakuwa vigumu kushiriki kupiga kura. Hivyo, ni muhimu Watanzania wakakamilisha haki yao ya msingi,” alieleza Jaji Mwambegele.
Nae Ofisa Mwandikishaji wa Jimbo la Mafia, Mohamed Othman, aliwahimiza wananchi waliojiandikisha katika awamu ya kwanza waendelee kujitokeza kuhakiki taarifa zao mapema bila kusubiri siku za mwisho za zoezi hilo.
Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa 16 nchini Tanzania inayoendelea na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kati ya mikoa hiyo, 11 ipo Tanzania Bara na mitano ipo Zanzibar, “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi wa Uchaguzi Bora.”