Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Sekta ya madini nchini Tanzania imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua inayotajwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi mmoja mmoja.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa tathmini ya sekta hiyo uliofanyika katika Hoteli ya Serena, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema mafanikio hayo yametokana na maono ya mbali na uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia katika kufungua milango ya uwekezaji na kuimarisha usimamizi katika sekta ya madini.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, bajeti ya Wizara ya Madini imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 89 hadi Shilingi bilioni 294 kwa mwaka wa fedha 2024/25, ongezeko linaloonesha dhamira ya serikali katika kuboresha miundombinu ya sekta hiyo, ikiwemo ujenzi wa maabara za kisasa na kuimarisha Kituo cha Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST).
“Sekta ya madini sasa ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wa Taifa. Tunaweza kusema kwa hakika kwamba madini ni maisha na madini ni utajiri kwa Watanzania,” alisema Waziri Mavunde, akisisitiza dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali hiyo muhimu.
Aliongeza kuwa mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 9.0 mwaka 2022/23 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024/25, hatua aliyoieleza kama “mapinduzi ya kweli” yaliyopatikana ndani ya muda mfupi.
Katika mwaka wa fedha 2023/24, mapato yatokanayo na sekta ya madini yameongezeka maradufu, ambapo Wizara ya Madini ilichangia zaidi ya Shilingi trilioni 2.1 katika mapato ya ndani ya serikali, mafanikio ambayo Waziri Mavunde alisema yanatokana na utekelezaji wa sera thabiti chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.
Serikali, alisema, itaendelea kuboresha mazingira rafiki kwa wachimbaji wa madini wa ngazi zote—wadogo, wa kati na wakubwa—kwa kuwapatia mitaji, mafunzo na masoko ya uhakika.
“Tumepiga hatua kubwa katika ufuatiliaji wa shughuli za uchimbaji kupitia mifumo ya kidigitali ambayo inasaidia kudhibiti utoroshwaji wa madini na kuongeza ukusanyaji wa mapato,” aliongeza.
Katika jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, Waziri alieleza kuwa Tanzania inaendelea kuvutia wawekezaji wa kimataifa, hatua inayoiweka nchi miongoni mwa maeneo bora ya uwekezaji wa madini barani Afrika.