
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amekemea vikali tabia chafu ya baadhi ya waganga wa jadi kuwaingilia kimwili wanawake kwa kisingizio cha kuwapatia tiba za kienyeji, na baadaye kuwafanya mateka kwa kuwarekodi wakati wa vitendo hivyo na kuwatishia kuwadhalilisha iwapo hawatatoa maslahi binafsi.
Kamanda Jongo ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, katika Kata ya Nyakagomba wilayani Geita, iliyolenga kusikiliza kero za wananchi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa vitendo hivyo vinachafua taswira ya waganga wa jadi wanaofanya kazi zao kwa uaminifu, na kwamba vyombo vya usalama havitasita kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika kujihusisha na matendo hayo ya kihalifu yanayohatarisha amani ya jamii.