Dar es Salaam
Muandaaji wa matamasha ya kidini ya Pasaka na Krismasi, Alex Msama, amewataka viongozi wa dini nchini kuhakikisha kuwa nyumba za ibada zinabaki kuwa maeneo ya kuhubiri maadili, amani, na upendo — badala ya kuwa majukwaa ya mijadala ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msama alisema kuwa ni muhimu kwa wachungaji na viongozi wote wa dini kuheshimu mamlaka zilizopo, kwa kuwa mamlaka hizo zimetajwa katika maandiko matakatifu kuwa zimewekwa na Mungu.
“Huwezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja,” alisema Msama. “Iwapo umechagua kuwa mtumishi wa Mungu, basi jitokeze wazi katika wito huo na uachane kabisa na siasa. Viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri injili, kuwahimiza watu kuacha maovu na kumrudia Mungu, siyo kuchochea mijadala ya kisiasa.”
Ameongeza kuwa katika kitabu cha Warumi 13, maandiko yanasisitiza kuwa yeyote anayepinga mamlaka zilizowekwa, anapinga pia mpango wa Mungu.
“Maandiko yanasema wazi kuwa washindanao na mamlaka wanashindana na Mungu mwenyewe, si tu viongozi waliopo madarakani. Kwa hiyo si vyema kwa watumishi wa madhabahu kushiriki katika harakati au matamko yanayodhalilisha mamlaka halali,” alifafanua Msama.
Amesisitiza kuwa jukumu la msingi la viongozi wa dini ni kuhakikisha taifa linadumu katika misingi ya upendo, mshikamano, na amani, kwa kutumia nafasi yao kuwahimiza waumini kuwa raia wema na watii wa sheria.