Na Silivia Amandius.
Missenyi, Kagera
Mchumi na mkulima kutoka mkoani Kagera, Evance Emmanuel Kamenge, ametangaza rasmi nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Missenyi—jimbo ambalo hapo awali lilijulikana kama Nkenge. Akiwa na maono ya kuleta mabadiliko chanya kupitia uongozi wa vitendo, Kamenge alizungumza kwa kina katika mahojiano maalum kupitia redio moja ya mjini Bukoba, akieleza kuwa atachukua fomu ya kugombea tarehe 28 Juni 2025.
Katika maelezo yake, Kamenge alieleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi waliomchangia kwa hiari gharama za kuchukua fomu ya kugombea. Amesema hatua hiyo imeongeza ari na hamasa katika safari yake ya kisiasa, huku akiwashukuru wana Missenyi kwa moyo wao wa kujitolea.
“Nimejawa na shukrani nyingi kwa ndugu zangu wa Missenyi. Leo nimeona kupitia makundi ya mtandaoni zaidi ya watu mia moja wakiwa tayari kunichangia kwa moyo mmoja. Hili halikuwa jambo dogo – limenipa nguvu ya ziada na kunithibitishia kuwa nipo kwenye njia sahihi,” alisema Kamenge.
Amefafanua kuwa japokuwa alikuwa na uwezo wa kugharamia fomu hiyo binafsi, uungwaji mkono wa wananchi umempa msukumo mpya wa kuwatumikia kwa bidii. “Naomba mniombee kwa Mwenyezi Mungu ili safari hii ikamilike salama na matokeo yake yawanufaishe wana Missenyi wote,” aliongeza kwa hisia.
Kamenge alisisitiza kuwa mamlaka ya uongozi si jambo la kibinadamu pekee, bali ni takwa la Mungu. “Tukisoma Biblia na Qur’ani, tunaelewa kuwa mamlaka huwekwa na Mungu. Sisi tunafanya jitihada, lakini uamuzi wa mwisho ni wa Mungu,” alisema.
Alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kuendelea kumuunga mkono katika hatua zinazofuata, huku akisisitiza kuwa dhamira yake ni kuwatumikia kwa uaminifu na uwazi.