Katika hatua ya kuimarisha uwazi na ushirikishwaji wa wananchi, Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO) imeandaa mikutano maalum kati ya Wakuu wa Mikoa na waandishi wa habari, kwa lengo la kuwasilisha kwa umma mafanikio yaliyopatikana katika maeneo yao.
Akizungumza leo Juni 29, 2025 Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema mikutano hiyo itaanza rasmi Julai Mosi, 2025 na kufanyika hadi Julai 18, 2025 jijini Dodoma, ambapo kila Mkuu wa Mkoa atakuwa na fursa ya kueleza utekelezaji wa miradi na huduma zinazogusa wananchi.
“Mikutano hii ni muendelezo wa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu maendeleo katika maeneo yao,” amesema Msigwa.
Kwa mujibu wa ratiba, Mkuu wa Mkoa wa Kagera ataanza mkutano Julai 1, akifuatiwa na Katavi (Julai 3), Singida (Julai 4) na Geita (Julai 9). Mikoa mingine itakayohusika ni Arusha, Tabora, Shinyanga, Tanga, Simiyu na Mwanza.
Msigwa amesisitiza kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), redio na televisheni mbalimbali, pamoja na mitandao ya kijamii na chaneli ya Maelezo TV, vitarusha matangazo hayo mubashara, ili kila Mtanzania aweze kushuhudia na kupata taarifa hizo moja kwa moja.
“Tunawaomba wananchi kufuatilia matangazo haya ili wajue namna Serikali yao inavyotekeleza miradi ya maendeleo. Tumeshafanya maandalizi ikiwemo kuchukua picha, video na mahojiano na wananchi wanaonufaika, ambazo zitasambazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari,” ameongeza Msigwa.
Aidha, ametoa wito kwa Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha wanaratibu ushiriki wa viongozi na maafisa wa mikoa yao kikamilifu ili kufanikisha lengo kuu la kutoa taarifa kwa umma.