
Na mwandishi wetu, Simanjiro
MBUNGE wa Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka na mbunge wa Afrika Mashariki James Ole Millya wamekutana kwenye ofisi ya CCM wilaya ya Simanjiro walipofika kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge.
Kwa nyakati tofauti wanasiasa hao nguli katika wilaya ya Simanjiro wamewahi kunyang’anyana ubunge mwaka 2015/2020 na mwaka 2020/2025.
Mwaka 2015 James Ole Millya akiwa Chadema alimbwaga kwa Ole Sendeka kwa kumtoa katika nafasi hiyo na mwaka 2020 Ole Sendeka alimbwaga Ole Millya na kurejea kwenye ubunge wake
Wanasiasa hao wawili wenye ushawishi mkubwa katika siasa za wilaya ya Simanjiro wamekutana Juni 30 mwaka 2025 kwenye ofisi za CCM za wilaya hiyo.
Ole Millya alitangulia kufika kwenye ofisi za CCM saa nne na dakika 11 asubuhi na Ole Sendeka akafika saa nne na dakika 20 hivyo akasubiri mwenzake atoke ndani ndipo akaingia ofisini kuchukua fomu.
Kila mmoja kwa wakati wake walionyesha risiti za malipo ya Sh500,000 ya gharama za kugombea ubunge na kupatiwa fomu hizo na Katibu wa CCM wilaya hiyo Amos Shimba.
Kila mmoja kwa nyakati tofauti hawakuwa tayari kuzungumza chochote kwa waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa fomu zaidi ya kupiga picha.
Ole Millya alijaza fomu na kurejesha saa tisa alasiri Julai 30 mwaka 2025 huku Ole Sendeka akieleza kuwa atarejesha fomu zake Julai mosi mwaka 2025.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro Amos Shimba akiwakabidhi fomu zao kwa nyakati tofauti ameeleza kwamba mwisho wa kurejesha ni Julai 2 mwaka 2025 saa 10 alasiri.
“Mwisho wa kurejesha ni Julai 2 mwaka 2025 na mtu ambaye atashindwa kurejesha kwa wakati atakuwa amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha uteuzi wa nafasi ya ubunge,” amesema Shimba.
Baadhi ya waliochukua fomu ya ubunge ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer na mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia wilaya ya Simanjiro, Lenana Lenganasa Soipey.
Wengine waliochukua fomu ni mwalimu Mwajuma Bakari Ally, mkurugenzi wa shule ya msingi New Vision ya mji mdogo wa Mirerani Prisca Msuya na mwanasheria wa kujitegemea Ibrahim Wambura Majura.
Pia, wapo Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Simanjiro Timoth Lengitambi, mwenyekiti wa shirika la wateule wa Mama Tanzania (Wamata) Lekoko Ngitiri, Mathayo Londross na katibu wa CWT wilaya ya Simanjiro, mwalimu Jonathan Losioki.