NA DENIS MLOWE,
TIMU ya Soka ya Mlowa Fc imemaliza msimu kwa kishindo, ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao Timu ya soka ya Ilolo Mpya fc katika dabi ya Jimbo la Ismani iliyosubiriwa kwa hamu kubwa na maelfu ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia fainali ya mashindano ya kombe Sabasaba Super Cup.
Ushindi huu unaifanya Mlowa fc kutawazwa rasmi mabingwa wa mashindano hayo ya Sabasaba Super Cup 2025 yaliyodhaminiwa na Mkuu wa wilaya Mstaafu wa Monduli Festo Kiswaga aliyeweka milioni 10 msimu huu kwa ajili ya mashindano hayo.
Katika mchezo huo uliopigwa dakika 90 timu ya Mlowa fc walijipatia magoli yao kila kipindi kwa goli la mfungaji bora wa mashindano hayo Fadhili Malenda na goli la pili walijifunga Ilolo mpya baada ya kushindwa kuokoa mpira uliokuwa ikielekea golini kwao na beki kujifunga
Licha ya kupoteza mchezo huo Ilolo mpya watajilaumu wenyewe kwa kukosa magoli mengi ya wazi kutokana na paparapapara za washambulaji wao walipofika golini.
Fainali hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Ilolo Mpya na kushuhudiwa na mamia ya mashabiki mbele ya mdhamini wa mashindano hayo Festo Kiswaga ambaye aliambatana na mgeni rasmi kutoka Mbuga ya wanyama ya Ruaha , Mhifadhi Jabir Ndagula ambaye alikabidhi kitita cha milioni 3 kwa bingwa.
Wakizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi Mratibu wa mashindano hayo, Dc mstaafu Festo Kiswaga na mgeni rasmi, katibu wa chama cha soka wilaya ya Iringa mjini, Yahaya Mpelembwa walisema lengo limetimia kuibua vipaji.
Mratibu Yustino Mdesa alisema kuwa wanashukuru kwa mdhamini Festo Kiswaga kudhamini mashindano hayo kwa miaka 10 tangu 2022 hadi 2030 kwa kila mwaka kupandisha zawadi za ushindi na kuwashukuru wadhamini wengine waliojitokeza wakiwemo benki ya NMB na Ruaha national park.
Alisema katika mashindano ya mwaka huu wameongeza zawadi tofauti na msimu uliopita ambapo kwa sasa bingwa wa mashindano hayo ataibuka na kitita cha milioni 3 zilizotolewa na Festo Kiswaga.
Awali mdhamini Festo Kiswaga ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Ccm kutokea Iringa Vijijini alisema kuwa mashindano hayo kwa mwakani udhamini utaongezeka ambapo sh. Milioni 15 zitawekwa katika mashindano hayo.
Naye mgeni rasmi , Jabir Ndagula alimpongeza mdhamini mkuu wa mashindano hayo Festo Kiswaga kwa kuwezesha mashindano hayo na vipaji kuonekana na kusema kuwa yamekuwa mashindano ambayo yanawakusanya vijana na kupunguza ujangiri na kuongeza kuwa kama Ruaha wamechukua fursa hiyo na wao kuweka mkono katika kutoa elimu ya uhifadhi kwa vijana.
Licha ya Bingwa kuibuka na kitita milioni 3 mshindi wa pili aijipatia timu ya Ilolo Mpya sh 1,500,000 mshindi wa tatu timu ya Mboliboli fc laki 7 wakati timu yenye nidhamu Mbingama fc sh.laki 2,Mfungaji bora Fadhili Malenda laki 1 ,kipa Bora Justin Kambanga laki 1
Katika mashindano hayo kwa upande wa wanawake bingwa alikuwa Ukwega Girls Fc waliibuka na sh laki 2 wakati mshindi wa pili Ilolo girls walipata sh laki 1







