NEWCASTLE: KLABU ya Newcastle United imekamilisha usajili wa beki wa kati wa timu ya taifa ya Ujerumani Malick Thiaw kutoka ligi kuu ya Italia Serie A kunako klabu ya AC Milan.
Thiaw mwenye miaka 24 anajiunga na Newcastle kama usajili wa tatu msimu huu kwa ada ya uhamisho inayokadiriwa kufikia thamani ya karibu pauni milioni 34.6 baada ya winga Anthony Elanga kutoka Nottingham Forest na golikipa Aaron Ramsdale aliyetua kwa mkopo kutoka Southampton.
Beki huyo alikuwa sehemu muhimu ya safu ya ulinzi ya AC Milan msimu uliopita akihusika kwenye mechi 31 za mashindano yote lakini ilionekana mara chache sana katika michezo ya mwisho wa msimu wa Serie A klabu hiyo ikimaliza vibaya ligi hiyo wakiwa nafasi ya 8.
Meneja wa Newcastle Eddie Howe alinukuliwa katika taarifa ya klabu hiyo akielezea furaha yake na kusema kuwa amemfuatilia beki huyo kwa muda mrefu na kuridhishwa na kiwango chake huku akiamini ujio wake klabuni hapo utaongeza ubora wa safu yake ya ulinzi.
Newcastle iliyomaliza msimu katika nafasi ya tano msimu uliopita na kupata nafasi kwenye Ligi ya Mabingwa wataanza kampeni yao ya Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa Jumamosi.
The post Newcastle yang’oa kitasa cha AC Milan first appeared on SpotiLEO.