UDINE: GOLIKIPA namba moja wa mabingwa wa Ulaya Paris St Germain Gianluigi Donnarumma ameandika barua kwa mashabiki wa klabu hiyo akithibitisha kuondoka kwake PSG baada ya kuondolewa kwenye kikosi hicho na meneja wake Luis Enrique aliyemuacha kipa huyo raia wa Italia nje ya kikosi cha UEFA Super Cup.
Katika barua ya wazi kwa mashabiki wa klabu hiyo Donnarumma amelaumu kile alichokiita maamuzi ya mtu mmoja kama sababu kubwa ya Mlinda lango huyo kufkia maamuzi ya kuondoka katika klabu hiyo baada ya kudumu kwa miaka minne.
Katika barua hiyo Donnarumma ameandika-.
“Kwa mashabiki maalum wa Paris,
Tangu siku ya kwanza nilipowasili, nilijitoa kwa kila kitu ndani na nje ya uwanja kupambania nafasi yangu klabuni hapa na kulinda lengo la klabu yetu ya Paris Saint-Germain. Kwa bahati mbaya, mtu fulani aliamua kuwa siwezi tena kuwa sehemu ya kikosi na kuendelea kuchangia mafanikio ya timu nimekatishwa tamaa na kuvunjwa moyo.
Natumai nitapata fursa ya kuwatazama mashabiki wetu ndani ya uwanja wetu wa Parc des Princes kwa mara nyingine na kuwaaga kama inavyopaswa kufanywa. Hilo lisipotokea, nataka mjue kwamba ‘sapoti’ yenu na mapenzi yenu kwangu yanamaana kubwa na sitasahau kamwe.
Daima nitabeba kumbukumbu za hisia zote, siku zetu za maajabu, na ninyi ambao mmenifanya nijisikie nyumbani. Kwa wachezaji wenzangu, familia ya pili, asante kwa kila vita tulopigana pamoja, kila kicheko, kila wakati tulioshirikiana. Nyinyi ni ndugu zangu daima. Kuichezea klabu hii na kuishi katika jiji hili imekuwa heshima kubwakwangu. Asante, Paris”
Donnarumma mwenye umri wa miaka 26 alichangia pakubwa katika kampeni ya PSG ya kushinda mataji matatu (treble) msimu uliopita, na kuwasaidia kushinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia. Bado haijawa wazi atatimkia wapi lakini tayari anahusishwa kuhamia ligi kuu ya England.
The post Donnarumma aacha lawama kwa Enrique akiaga PSG first appeared on SpotiLEO.