DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva Abdul Idd ‘Lava Lava’, amevunja ukimya na kuelezea kwa uchungu changamoto zinazomkumba kila anapotoa kazi mpya ya muziki.
Kupitia ujumbe wake uliosheheni hisia nzito, Lava Lava amesema kuwa kuna watu ambao hufanya fitina kila mara anapotangaza au kuachia nyimbo zake mpya.
Amedokeza kuwa hali hiyo imejionyesha wazi zaidi baada ya kuachia EP yake mpya inayokwenda kwa jina la Time EP, akisema ni kama kuna nguvu za kukwamisha juhudi zake kila mara anapojaribu kusonga mbele kimuziki.
Pamoja na hali hiyo, msanii huyo wa lebo ya WCB amebaki na moyo wa matumaini, akisema, “Ila Mungu yupo na mimi”, kauli inayodhihirisha imani yake kuwa, licha ya vizingiti anavyopitia, bado anaamini kuwa haki na juhudi zitashinda.
Kauli ya Lava Lava inatoa picha halisi ya mazingira ya ushindani mkali na wakati mwingine usio wa haki unaowakumba wasanii wengi nchini.
Hali hii huenda ikaathiri sio tu kazi zao za sanaa, bali pia hali yao ya kisaikolojia na maendeleo kwa ujumla.
Mashabiki wake wameonyesha kuunga mkono hisia zake, huku wengi wakimtia moyo kuendelea kufanya kazi na kuamini kuwa ukweli utajitokeza muda si mrefu.
The post Lava Lava afunguka: “Nafanyiwa fitina kila nikitoa muziki mpya” first appeared on SpotiLEO.