DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hemed Morocco, amesema kikosi chake kimejipanga kwa umakini wa hali ya juu kuelekea mchezo wa hatua ya robo fainali dhidi ya Morocco
Akizungumza Dar es Salaam leo Morocco amesema Stars imefanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika michezo ya awali na sasa wachezaji wako imara kiakili, kimwili na kimbinu.
“Tumeiangalia sana Morocco kupitia michezo yao na tukafanya marekebisho uwanjani. Ni ngumu kucheza nao kama hujawafuatilia. Lakini kwa wachezaji tulionao, tuna wachezaji waliokomaa na wenye uzoefu, tumerekebisha kasoro na tuko tayari kupambana,” amesema.
Kocha huyo aliongeza kuwa Morocco ni timu yenye hadhi na ubora mkubwa barani Afrika, lakini Stars itaingia kwa heshima na ari ya kupambana ili kupata matokeo chanya.
“Morocco ni timu nzuri, tutaingia kwa kuwaheshimu na naamini nao wanatuheshimu. Utakuwa mchezo wa aina yake na tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri ili kuipa furaha Tanzania,” alisisitiza Morocco.
Kwa upande wake, beki mkongwe Shomari Kapombe amesema wachezaji wote wako tayari kwa asilimia 100 kuhakikisha Taifa Stars inafanya vizuri.
“Tunajua mpinzani ni mzuri, na hiyo inatupa morali na changamoto ya kujituma zaidi. Huu utakuwa mchezo wa tofauti na tutajitolea kwa uwezo wetu wote ili kuleta matokeo mazuri,” alisema Kapombe.
Taifa Stars inatarajiwa kushuka dimbani kesho kutegemea ikiwa na malengo ya kuipa zawadi Watanzania kupitia ushindi muhimu dhidi ya Morocco.
The post Taifa Stars kuivaa Morocco kimbinu first appeared on SpotiLEO.