MAREKANI:MSANII wa kimataifa kutoka Marekani, Ciara, ameachia rasmi wimbo wake mpya unaoitwa ‘Low’, aliomshirikisha mkali wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’. Uzinduzi wa wimbo huu umeibua mjadala mpya kuhusu nafasi ya waandishi wa nyimbo katika muziki wa kisasa.
Katika ulimwengu wa muziki, uandishi wa nyimbo ni kazi rasmi inayolipwa vizuri, tofauti na mtazamo wa baadhi ya watu wanaoona kuandikiwa nyimbo kama udhaifu. Wimbo wa Low ni mfano halisi wa jinsi ambavyo ubunifu wa pamoja unavyoweza kuleta kazi ya kiwango cha juu.
Wimbo huu umeandikwa na waandishi wanane, akiwemo Diamond Platnumz mwenyewe pamoja na Ciara. Majina mengine ya waandishi ni Charlotte Wilson, Courtlin Jabrae, Darius Logan, Dominique Logan, Magnus Klausen, na Ebenezer Fabiyi, ambaye pia ndiye mtayarishaji wa wimbo huo.
Kwa Diamond Platnumz, huu ni ushindi mkubwa sio tu kama msanii aliyetumika katika wimbo wa kimataifa, bali pia kama mwandishi aliyechangia moja kwa moja kwenye uundwaji wa mashairi ya wimbo huo. Hii inaweka jina lake kwenye orodha ya waandishi wa muziki katika albamu inayowakutanisha mastaa wakubwa duniani kama Chris Brown, Busta Rhymes, na Lil Baby.
Mchango wa Diamond umeongeza ladha ya kipekee ya Bongo Fleva katika muziki wa kimataifa, na kuthibitisha kuwa wasanii wa Afrika, hususan Tanzania, wana nafasi kubwa kwenye jukwaa la dunia.
Kwa msingi huo, ni dhahiri kuwa kuandikiwa au kushirikiana kuandika nyimbo siyo udhaifu, bali ni sehemu ya kazi ya sanaa inayotegemea ushirikiano wa vipaji mbalimbali. Wimbo wa Low ni ushahidi kuwa muziki bora ni zao la nguvu za pamoja, na nafasi ya Diamond katika kazi hii ni ya kihistoria kwa muziki wa Tanzania.
The post Diamond angara kimataifa kwenye wimbo mpya na Ciara ‘low’ first appeared on SpotiLEO.