STOCKHOLM: Mshambuliaji wa Newcastle United Alexander Isak ametajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Sweeden wakati huu taifa hilo likijiandaa kucheza mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026, licha ya kuwa hajaichezea Newcastle msimu huu anapotafuta njia ya kuondoka.
Jina la Mshambuliaji huyo ni sehemu ya kikosi cha wachezaji 24 kilichoitwa na kocha mkuu wa timu ya taifa ya Sweeden Jon Dahl Tomasson kwa ajili ya michezo dhidi ya Slovenia na Kosovo itakayopigwa baadae mwezi Septemba.
“Nina furaha sana kwamba Alexander Isak anataka kuwa kwenye kikosi, ni mchezaji mkubwa. Hali aliyonayo si nzuri na hajafanya mazoezi na timu. Lakini ni mchezaji anayeweza kuamua mechi na anataka kuwa sehemu ya kikosi chetu. Kombe la Dunia ni muhimu kwa Alexander Isak.” – Tomasson amesema.
Isak, mmoja wa washambuliaji mahiri duniani, hajawa sehemu ya kikosi cha Newcastle kwa mechi mbili za Premier League dhidi ya Aston Villa na Liverpool na anafanya mazoezi mbali na kikosi cha kwanza.
Uongozi wa timu ya taifa ya Sweeden umesema Isak anatarajiwa kuungana na timu hiyo ya taifa mjini Stockholm Jumatatu, siku ambayo dirisha la usajili litakuwa linafungwa.
The post Isak aitwa Sweeden first appeared on SpotiLEO.