KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua jijini Cairo, Misri kujiandaa na msimu mpya wa mashindano, lakini kuna straika mmoja aliyesajiliwa hivi karibuni ametua jijini Dar es Salaam ili kuisubiri timu hiyo itakaporejea nchini kwa ajili ya Tamasha la Simba Day.
Tamasha hilo la Simba litafanyika Septemba 10, siku chache kabla ya kucheza mechi ya Ngao ya Jamii kuzindua msimu wa 2025-2026 dhidi ya watani zake wa jadi itakayopigwa Septemba 16 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ipo hivi. Simba ilishakamilisha usajili wa mshambuliaji wa Wydad Casablanca ya Morocco, Seleman Mwalimu ‘Gomes’ kwa mkopo wa msimu mzima baada ya kukitumikia kikosi hicho kwa miezi sita tangu alipojiunga nacho Januari 2025.
Gomes alisajiliwa na Wydad kupitia dirisha dogo akitokea Fountain Gate aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo kutokea Singida Black Stars, na akaandika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza fainali za Kombe la Dunia la Klabu 2025 zilizofanyika Marekani kati ya Juni 15 hadi Julai 13, 2025.
Taarifa zinasema kwamba, Gomes aliwasili juzi usiku nchini akitokea Morocco ili kujiunga na kikosi cha Simba kitakachorejea wiki ijayo kutoka Misri kilikoweka kambi. Awali kilikuwa jijini Ismailia kabla ya kuhamia Cairo kilipo kwa sasa.
Chanzo cha kuaminika kilicho karibu na mchezaji huyo kimethibitisha kwamba Gomes aliwasili nchini kwa ajili ya kusubiri kikosi hicho kurejea kikitokea Misri kilipoweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya na muda wowote kuanzia leo anaweza kutambilishwa.
“Lengo lilikuwa ni kumtambulisha Misri na wachezaji wenzake, lakini kuna mambo ambayo hayakwenda sawa kama tulivyopanga. Ni kweli amewasili Tanzania kwa ajili ya kukamilisha taratibu zote za utambulisho kikosini,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema kuwa, sababu ya kutojumuika na wachezaji wenzake nchini Misri ni kutokana na kikosi hicho kurejea nchini mwishoni mwa mwezi huu, hivyo kilichofanyika ni kuandaa taratibu za kuhakikisha anarudi Tanzania.
Mshambuliaji huyo ndiye wa kwanza kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco baada ya kuonyesha kiwango bora wakati akiwa Fountain Gate, ambako hadi anaondoka dirisha dogo la Januari mwaka huu, alikuwa amefunga mabao katika Ligi Kuu Bara.
Nyota huyo alijiunga na Fountain akitokea Singida Black Stars iliyomsajili kutokea KVZ ya Zanzibar ambapo msimu wa 2023-2024 alikuwa mfungaji bora akitupia mabao 20 na kutoa asisti saba katika mechi 27 kati ya 30 alizocheza.
Gomes alikuwa ni mchezaji wa kwanza kutoka Ligi Kuu Bara na kwenda kujiunga na Wydad kwa msimu wa 2024-2025, baada ya aliyekuwa kiungo nyota wa Yanga, Stephane Aziz KI, kujiunga na kikosi hicho kufuatia kukitumikia kwa misimu yake mitatu.
Gomez anakuwa mshambuliaji wa pili kujiunga na Simba msimu huu, baada ya Jonathan Sowah aaliyetambulishwa akitokea Singida Black Stars na liyeonyesha kiwango bora tangu ajiunge na timu hiyo dirisha dogo la Januari 2025.
Sowah tangu ajiunge na Singida dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya ana alifunga jumla ya mabao 14 katika mechi zote 15 za mashindano kati ya mabao hayo 13 ni ya Ligi Kuu Bara na jingine na Kombe la FA, timu hiyo ikifika fainali na kulala kwa Yanga.
Ujio wa Gomez ndani ya kikosi hicho, unaongeza vita mpya katika eneo la ushambuliaji, ambapo mbali na Sowah ila yupo pia Mganda Steven Mukwala ambaye kwa msimu uliopita wa 2024-2025, aliifungia Simba mabao 13 ya Ligi Kuu Bara.
Usajili wa Gomez unaifanya Simba kufikisha wachezaji wapya 10 baada ya Rushine De Reuck, Neo Maema (Mamelodi Sundowns), Alassane Kante (Club Athletique Bizertin), Morice Abraham (FK Spartak Subotica) na Semfuko Charles kutoka Coastal Union.
Wengine ni Jonathan Sowah (Singida BS), Mohammed Bajaber (Kenya Police FC), Anthony Mligo (Namungo FC) na Naby Camara aliyetokea Al-Waab SC ya Qatar ili kuipigania timu hiyo baada ya kukosa taji la Ligi Kuu kwa misimu minne mfululizo.
The post HUKO SIMBA VYUMA BADOOH…..MASHINE MPYA HII HAPA…IMECHEZA KOMBE LA DUNIA LA KLABU… appeared first on Soka La Bongo.