DAR ES SALAAM: SINGIDA Black Stars FC itaanza kampeni yake ya michuano ya CECAFA Kagame Cup 2025 leo Jumanne kwa kuvaana na Ethiopian Coffee SC kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo
Huo utakuwa ni mtihani wa kwanza kwa kocha mkuu mpya Miguel Gamondi tangu kujiunga nao msimu huu
Mchezo huo wa Kundi A utachezwa baada ya pambano la ufunguzi kati ya Kenya Police FC na Garde Cotes FC ya Djibouti mchana saa 7.
Gamondi, ambaye aliwahi kufundisha Yanga amesema michuano hiyo ni nafasi muhimu ya kuandaa kikosi chake kuelekea kwenye michuano ya Ligi Kuu na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Michuano hii inanipa nafasi ya kujaribu wachezaji kadhaa tunapojiandaa kwa Kombe la Shirikisho la CAF na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania,” alisema Gamondi.
Singida Black Stars itategemea zaidi ubora wa wachezaji wapya akiwemo kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama aliyesajiliwa kutoka Yanga, pamoja na Khalid Aucho wa Uganda atakayekutana na timu baada ya majukumu ya timu ya taifa (Uganda Cranes).
Kocha wa Ethiopian Coffee, Abiy Kassahun, alisema timu yake ipo tayari kwa changamoto.
CECAFA Kagame Cup 2025 imevutia jumla ya timu 12, ikiwa na Betika kama mdhamini mkuu, Times FM ya Tanzania kama mshirika, huku Rais wa Rwanda Paul Kagame akiendelea kuwa mlezi na mdhamini wa mashindano haya ya kihistoria.
The post Mtihani wa Gamondi Leo dhidi ya Ethiopian CECAFA first appeared on SpotiLEO.