VADUZ: NAHODHA mpya Youri Tielemans aliingia kambani mara mbili timu ya taifa ya Ubelgiji ikiibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Liechtenstein mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 katika Uwanja wa Rheinpark Stadion mjini Vaduz huku winga Malick Fofana akifunga bao lake la kwanza la kimataifa.
Maxim De Cuyper, Arthur Theate na Kevin De Bruyne pia walifunga mabao katika mchezo ambao ulitawaliwa na Ubelgiji ambayo ingepata ushindi mkubwa zaidi kama ingetumia kila nafasi iliopata.
Ushindi huo umewafanya kufikisha pointi saba katika mechi tatu za kufuzu kombe la Dunia hadi sasa na kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi hilo, pointi tatu nyuma ya vinara Wales lakini wakiwa na michezo miwili mkononi. Liechtenstein wako mkiani wakiwa hawana hata pointi moja katika mechi 4 walizocheza.
Ilibidi Ubelgiji wasubiri dakika 29 kupata bao lao la kwanza licha ya kutengeneza nafasi nyingi huku De Cuyper akiunganisha kwa kichwa krosi ya Thomas Meunier kutoka upande wa kulia, kabla ya Theate kuachia shuti kali la umbali wa mita 27.
Ilikuwa 1-0 wakati wa mapumziko, lakini ndani ya dakika moja ya kipindi cha pili, Tielemans aliingiza mpira mzuri kutoka mita 22 nje kidogo ya lango na kufunga bao hilo mnamo dakika ya 46
Theate alifunga bao lake la kwanza la kimataifa alipoweka nyavuni kwa kichwa krosi ya De Cuyper, na De Bruyne akimalizia vyema pasi ya Hans Vanaken na kufanya matokeo kuwa 4-0.
Tielemans alifunga la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 70 kisha bao la dakika za lala salama la Fofana katika mechi yake ya pili ya kimataifa alipomalizia kazi nzuri ya Ubelgiji.
The post Tielemans aiongoza Ubelgiji kuivuruga Liechtenstein first appeared on SpotiLEO.