Na Farida Mangube, Morogoro
Wakulima nchini wametakiwa kuzingatia kilimo hai na endelevu ili kulinda afya za watu, mazingira, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na matumizi ya kilimo kisicho salama.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili katika Kampasi ya Edward Moringe, Morogoro, Machi 13-14, 2025, Prof. Samwel Kabote, Rasi wa Ndaki ya Sayansi ya Jamii na Insia wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), alisema kilimo hai kina mchango mkubwa katika ustawi wa jamii na usalama wa chakula.
Warsha hiyo inalenga kujadili mbinu za kuhamasisha na kuendeleza kilimo hai kwa wakulima, ikishirikiana na vijana kutoka taasisi za elimu na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Kabote alisema SUA, kupitia Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE), itaendelea kufanya tafiti na kutoa elimu ya ugani kwa wakulima ili kuwawezesha kulima kwa tija na kupata masoko ya bidhaa zao.
Aidha, alibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa inayokwamisha maendeleo ya kilimo hai ni ukosefu wa sera madhubuti, lakini watafiti wanaendelea kuishawishi serikali kutumia matokeo ya tafiti ili kuimarisha mfumo wa kisera wa sekta hiyo.
Kwa upande wake, Dkt. Adolf Makauki wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambaye pia ni mwenyekiti wa maandalizi ya warsha hiyo, alisema mwitikio wa wakulima kuelekea kilimo hai bado ni mdogo, lakini kuna matumaini ya ukuaji wake kadri elimu inavyoendelea kutolewa.
“Kilimo hai kinarudisha jamii katika mfumo wa kilimo wa asili, kabla ya kuanza matumizi ya kemikali. Tukitangaza zaidi faida zake, wakulima watahamasika kushiriki kwa wingi, kwani hakuna mtu anayependa kuugua magonjwa kama kisukari,” alisema Dkt. Makauki.
Naye Dkt. Lilian Sechambo, Mhadhiri wa Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani, SUA, alisema kilimo hai ni msingi wa ustawi wa jamii yoyote kwa kuwa hakitumii kemikali hatarishi, hivyo kusaidia kulinda afya za watu na mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Warsha hiyo inatarajiwa kufanya ziara kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro yanayotekeleza kilimo hai ili kubaini changamoto zilizopo na kubuni mikakati ya kuboresha sekta hiyo kwa manufaa ya taifa.