Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Same, Machi 13, 2025 – Goodness Grayson Ketto ameishukuru Hospitali ya Wilaya ya Same kwa huduma bora alizopata wakati wa kujifungua mtoto wake njiti, akisema kwamba uangalizi mzuri wa madaktari na wauguzi ulimsaidia yeye na mtoto wake kuimarika kiafya.
Katika mahojiano maalum na Fullshangwe Media, Goodness alieleza jinsi alivyokuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na hali ya mtoto wake, lakini wahudumu wa afya walimhakikishia usalama na kumpa matibabu bora.
“Nilikuwa na hofu kubwa kwa sababu mtoto wangu alikuwa njiti, lakini wauguzi walikuwa makini sana. Hali yangu imeimarika, na mtoto wangu sasa anaendelea vizuri,” alisema Goodness kwa furaha.
Aidha, aliushukuru uongozi wa hospitali hiyo, ukiongozwa na Mganga Mkuu, Dkt. Alexander, kwa kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali muhimu wakati wa kujifungua kwake, hatua iliyomuwezesha kupata huduma bora bila changamoto yoyote.
“Shukrani nyingi kwa uongozi wa hospitali hii, walifanya kila linalowezekana kuhakikisha afya yangu na ya mwanangu zinalindwa,” aliongeza.
Goodness pia alitoa pongezi kwa serikali kwa kuimarisha huduma za afya katika hospitali za umma, hususan kwa kina mama na watoto wanaohitaji uangalizi maalum kama watoto njiti.
“Bila msaada wa serikali na hospitali hii, hali yangu ingekuwa ngumu zaidi. Nashukuru sana kwa msaada wao,” alisema huku akifurahia afya njema ya mtoto wake, ambaye sasa ana umri wa miezi saba.
Aliwataka wazazi kuacha kuhofia hospitali za serikali, akisisitiza kuwa zimeboreshwa sana na sasa zinatoa huduma bora zaidi hata kuliko baadhi ya hospitali binafsi.
“Hospitali ya Wilaya ya Same imepiga hatua kubwa, huduma zake ni bora zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma,” alisema Goodness na kuongeza:
“Mheshimiwa Rais anajitahidi sana kuboresha sekta ya afya, hasa kwa akina mama na watoto. Ombi langu ni kwamba serikali iendelee kupeleka vifaa tiba na dawa katika hospitali hii, kwani ni hospitali tegemezi kwa wakazi wa eneo hili.”
Huduma bora alizopata Goodness zimeongeza matumaini kwa familia yake na jamii kwa ujumla, zikionyesha mabadiliko makubwa katika sekta ya afya, hasa kwa wanawake na watoto wa Wilaya ya Same.