N’DJAMENA: MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga Celestin Ecua ameing’arisha timu yake ya taifa ya Chad kwa kuisawazishia bao katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Ghana ‘Black Stars’ jana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Ghana ilianza kupata bao la uongozi lililofungwa na Jordan Ayew kipindi cha kwanza.
Hata hivyo, dakika ya 89, Ecua alipiga shuti kali kwa mguu wa kushoto kutoka nje ya eneo la hatari, likamgonga mchezaji na kumpoteza kipa Benjamin Asare wa Ghana, na kuwafanya mashabiki wa Chad kushangilia kwa nguvu.
Sare hiyo imeifanya Chad kuambulia pointi moja lakini wakiendelea kushindi mkia kwenye Kundi I.
Black Stars walipoteza nafasi kadhaa za kufunga mapema, ambapo Antoine Semenyo wa Bournemouth na Mohammed Kudus wa Tottenham walikosa mabao wakiwa na nafasi nzuri.
Licha ya kupoteza pointi mbili, Ghana bado imebakia kileleni mwa Kundi I wakiwa na pointi tatu zaidi ya Madagascar, ambao waliibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mali nao wamejipatia uhai upya baada ya kuichapa Comoros mabao 3-0, na sasa wako pointi moja nyuma ya Madagascar.
Ni vinara wa makundi pekee watakaopata nafasi ya moja kwa moja kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Canada, Marekani na Mexico.
The post Ecua ang’ara Chad ikitoka sare first appeared on SpotiLEO.