BILBAO: HATIMAYE klabu ya Athletic Bilbao ya LaLiga imefanikiwa kumsajili tena beki wa kati mzaliwa wa Ufaransa Aymeric Laporte kutoka klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia baada ya FIFA kuidhinisha uhamisho wake.
Bilbao waliamua kumrejesha Laporte San Mames mapema mwezi Septemba lakini uhamisho huo haukukamilika kabla ya tarehe ya mwisho ya dirisha la usajili, huku vyombo vya habari vya Hispania vikiripoti kuwa Al-Nassr ndio waliokwamisha usajili huo kwa kwa kuchelewesha taarifa zake kwenye Mfumo wa Usajili wa FIFA.
Mapema mwezi huu, FIFA ilikataa ombi la shirikisho la soka la Hispania (RFEF) la kumpa upendeleo Laporte kwakuwa kosa lililokwamisha usajili wake halikuwa upande wa Bilbao bali linatokana na Al-Nassr.

Bilbao ilisema katika taarifa yake ya baadae Alhamisi kuwa wamepata idhini ya RFEF kuendelea na mazungumzo ya uhamisho wake kutoka Saudia kisha ikathibitisha kuwa hatua hiyo imekamilika, huku mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 akisaini mkataba wa miaka mitatu.
Laporte aliichezea Athletic Bilbao mechi 222 kabla ya kujiunga na Manchester City mwaka 2018, na kushinda mataji matano ya Ligi Kuu ya England, mawili ya Kombe la FA, matatu ya Carabao na moja la Ligi ya Mabingwa, kabla ya kuhamia Al-Nassr mwaka wa 2023.
Bilbao wanashika nafasi ya pili kwenye LaLiga wakiwa na ushindi wa mechi tatu katika mechi zote tatu walizocheza na watakuwa wenyeji Alaves kesho Jumamosi.
The post Laporte arudi LaLiga first appeared on SpotiLEO.






