LONDON: MENEJA wa Chelsea Enzo Maresca amesema Jeraha la fowadi wa timu hiyo Liam Delap ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa hapo awali na huenda likamuweka nje hadi Desemba.
Delap, ambaye alijiunga na Chelsea kutoka Ipswich Town kwa pauni milioni 30 mwezi Juni, alipata jeraha hilo katika mchezo dhidi ya Fulham kabla ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa na awali ilitarajiwa angekosa wiki sita hadi nane.
“Ni takriban wiki 10 hadi 12,” Maresca aliwaambia waandishi wa habari.
Huku akiwapa habari njema kuwa Cole Palmer, ambaye aliondolewa kwenye kikosi cha England kwa sababu ya jeraha la paja, amerejea mazoezini na ana nafasi ya kucheza dhidi ya Brentford.
“Cole alishiriki mazoezi ya jana kwa mara ya kwanza japo si mazoezi yote tuna kipindi kingine cha mazoezi leo mchana tutajaribu na tuone kama atakuwa sawa vinginevyo hatakuwepo”.
“Anapopatikana, tunahitaji kumsimamia na kudhibiti muda wake wa mechi kwa sababu ya wingi wa michezo.” amesema Maresca
Chelsea pia huenda wakampa nafasi mchezaji mpya Alejandro Garnacho, ingawa Maresca amesema winga huyo wa Argentina bado hajawa sawa kwa asilimia 100 baada ya kutocheza msimu huu kabla ya kuhama kutoka Manchester United.
The post Delap kurejea dimbani Desemba first appeared on SpotiLEO.