KOCHA wa Yanga, Romain Folz, amewataka wachezaji wa timu hiyo kusahau ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Simba na kugeukia mechi yao ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete de Benguela ya Angola.
Mara baada ya mchezo wa juzi wa Ngao ya Jamii kumalizika huku wachezaji wa timu hiyo wakiwa na furaha, Folz aliitisha kikao cha dharura na kuwataka wachezaji hao kusahahu ushindi huo na kuelekeza mawazo na nguvu zao kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezaji mmoja wa timu hiyo amesema kuwa baada ya mechi hio furaha yao ya kuifunga Simba ilikatishwa ghafla na Kocha Folz, alipowakumbusha kuwa wana mechi ngumu dhidi ya Wiliete na waache kushangilia mechi hiyo ya Ngao ya Jamii.
“Baada ya kuifunga Simba tulirudi vyumbani tukiwa na furaha kubwa, wenyewe tunashangilia, kocha Folz, alipoingia alikuta tunashangilia sana, akatuamuru tukae chini haraka, akatuambia ile ilikuwa mechi ya ‘bonanza’, tujiandae na mechi kamili ni dhidi ya Wiliete wikiendi hii, basi ikabidi tukae kimya wote,” alisema mchezaji huyo.
Alisema kocha huyo amewataka kuweka mkazo kenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa na kusahau ushindi wa Ngao ya Jamii.
Kikosi cha Yanga tayari kimetua nchini Angola tayari kwa mchezo huo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga itacheza mchezo huo leo kwenye uwanja wa 11 de Novembro, jijini Luanda saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na baadaye kurudiana jijini Dar es Salaam Septemba 27.
Wakati Simba na Yanga zikiwa zimeondoka nchini, Azam ilikuwa ya kwanza, Ijumaa iliyopita kwenda Juba, nchini Sudan Kusini kwa ajili ya mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya El Merrikh Bentiu, unaotarajiwa kuchezwa, Jumamosi, Uwanja wa Juba, nchini humo, saa 11:00 jioni kwa sasa za Tanzania.
The post FURAHA YA KIPIGO CHA SIMBA YAZIMWA GHAFLA YANGA…..FOLZ AWAPA ‘KIJEMBE’ MASTAA.. appeared first on Soka La Bongo.