DAR ES SALAAM: WEKUNDU wa Msimbazi Simba wanaingia dimbani leo saa 1:00 usiku kuwawinda Fountain Gate katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba wametoka katika mchezo wa kimataifa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United walioshinda ugenini bao 1-0.
Wanarudi kwenye ligi lakini watacheza mchezo huo bila Kocha Mkuu Fadlu Devis aliyetimka baada ya mchezo huo wa kimataifa hivyo, kibarua kipo kwa aliyekabidhiwa majukumu ya muda mfupi Hemed Morocco, Kocha Mkuu wa Taifa Stars.
Macho yote leo wataangalia aina kikosi kitakachopangwa, mfumo gani lakini jambo zuri Morocco ni Kocha anayeifahamu ligi ya Tanzania kwa kuwa muda mwingi hufuatilia.
Kwa ubora waliouonesha Simba katika mchezo wa kimataifa unategemewa utakuwa hivyo kwa mchezo wa ligi.
Ingawa wanakwenda kucheza na timu ikiwa na wachezaji 10 tu, kati ya hao makipa ni wawili.
Huenda Fountain Gate kikawakuta kilichowahi kuwatokea Kitayosce misimu miwili iliyopita ambao ni (Tabora United) kwa sasa TRA United iliyokutana na Azam FC ikiwa pungufu.
Katika mchezo huo wa kwanza msimu uliopita ambao Azam ilishinda mabao 4-0, Kitayosce iliingia na wachezaji wanane kufuatia changamoto ya usajili na mechi hiyo ilimalizika kikanuni dakika ya 15 baada ya wachezaji wawili wa Kitayosce kuumia na kushindwa kuendelea.
Pamoja na hayo, Fountain Gate haijawahi kuifunga Simba katika mechi sita walizokutana katika Ligi Kuu tangu timu hiyo ilipokuwa ikiitwa Singida Big Stars kisha kuwa Singida Fountain Gate baada ya kununuliwa.
Katika mchezo wake uliopita, Fountain imetoka kupoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City ikiwa ni mechi ya kwanza ya ligi msimu huu.
The post Simba kuwawinda Fountain Gate leo first appeared on SpotiLEO.