ST. PAULI: KOCHA Kasper Hjulmand wa Bayer Leverkusen amesema bado wako katika hatua ya ujenzi wa timu mpya akihitaji muda zaidi ili mipango yake klabuni hapo ikamilike, akiyasema hayo kwenye mkutano na wanahabari kuelekea mechi yao ya Bundesliga Jumamosi dhidi ya St. Pauli.
Leverkusen, washindi wa makombe mawili ya ndani mwaka 2024 chini ya kocha Xabi Alonso wakati huo, wamepata mtikisiko msimu huu baada ya kuondoka kwa mchezaji muhimu kama Florian Wirtz, Jonathan Tah, Granit Xhaka na Jeremie Frimpong.
“Ni mchakato. Tunahitaji muda na tunahitaji mechi, na zinakuja. Tuna matumaini makubwa na nadhani tuna timu yenye uwezo. Tunaweza kujenga kikosi bora, lakini bado tuko katika hatua ya ujenzi. Wachezaji wengi ni wapya, makocha ni wapya ndiyo hali ilivyo. Lakini katika kila mchezo, lazima tupate matokeo.” – Hjulmand alisema katika mkutano na waandishi wa habari
Kikosi hicho kiko nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi, kikiwa na pointi tano, saba nyuma ya vinara Bayern Munich baada ya mechi nne, na mbili nyuma ya St. Pauli waliopo nafasi ya tano.
Baada ya kufukuzwa kwa kocha Erik ten Hag baada ya mwanzo mbaya kwenye Bundesliga, Leverkusen walimteua Hjulmand Septemba 8. Tangu alipoanza, amepata ushindi mmoja na sare moja katika mechi zake mbili za ligi.
The post “Bayer Leverkusen tujenga Timu Mpya” – Kocha Hjulmand first appeared on SpotiLEO.