KILIMANJARO:OFISA Habari wa timu ya Polisi Tanzania Inspekta Frank Lukwaro, amesema wanatarajiwa kufanya kikao maalum na viongozi wa mashabiki kutoka maeneo mbalimbali ya mji wa Moshi Oktoba 1, 2025 kwa ajili ya kujadili maandalizi ya timu hiyo kuelekea michezo ya Ligi ya Championship.
Kikao hicho ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha ushirikiano kati ya klabu na mashabiki wake, hususan walioko katika mkoa huo ambapo michezo ya nyumbani inatarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Kwa mujibu wa Inspekta Lukwaro, lengo kuu la kikao hicho ni kuweka mikakati ya pamoja ya kuhamasisha mashabiki kuipa sapoti timu hiyo kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano.
Timu ya Polisi Tanzania FC imekuwa ikiweka nguvu kubwa katika maandalizi ya ndani na nje ya uwanja ili kuhakikisha inarejea Ligi Kuu kwa kishindo.
“Kama sehemu ya maandalizi ya timu, tunatambua umuhimu wa mashabiki wetu, hasa wale walioko nchi nzima hivyo kikao hiki kitatoa nafasi ya kuwasikiliza viongozi wao, kupeana taarifa rasmi za klabu, na kujenga mpango wa pamoja wa ushirikiano kuelekea mechi zetu za Championship,” alisema Inspekta Lukwaro.
Kikao hicho pia kinatarajiwa kugusia masuala kama vile uhamasishaji wa mashabiki kuhudhuria mechi, usalama, utaratibu wa usafiri kwa mashabiki, pamoja na nafasi ya chama cha soka mkoa wa Kilimnjaro (KRFA).
Aidha, viongozi wa mashabiki kutoka maeneo maarufu ya Njoro, Pasua, Chuo cha Ushirika wanatarajiwa kuhudhuria.
Polisi Tanzania FC inatumaini kuwa mashabiki wake wa Mkoa wa Kilimanjaro wataendelea kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya timu, na kupitia kikao hiki, matarajio ni kuibuka na mpango kazi madhubuti utakaosaidia kuipeleka timu hiyo katika mafanikio makubwa msimu huu.
The post Polisi kuteta na mashabiki zao first appeared on SpotiLEO.