Kocha Mkuu wa Benfica ya Ureno, Jose Mourinho, anarejea leo kwenye dimba la Stamford Bridge, uwanja wenye historia kubwa katika maisha yake ya soka. Safari hii anarejea kama mpinzani, akiiongoza Benfica kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya mabingwa wa dunia, Chelsea. Mourinho alitangazwa kuwa kocha mkuu wa Benfica wiki iliyopita na leo anakabiliwa na mtihani wake mkubwa wa kwanza akiwa na timu hiyo mpya.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Mourinho alisema anajihisi kama yupo nyumbani lakini sasa anawakilisha Benfica na lengo lake ni moja tu — kushinda. “Najihisi kama niko nyumbani, lakini ndani ya dakika 90 sitafikiria nilikotoka. Mimi si ‘The Blues’ tena, mimi ni mwekundu wa Benfica na nataka kushinda,” alisema.
Mourinho aliwahi kuinoa Chelsea katika vipindi viwili tofauti (2004–2007 na 2013–2015) na kuandika historia kwa kutwaa mataji makubwa ikiwemo ubingwa wa Ligi Kuu England mara tatu, Kombe la FA mara moja, Kombe la Ligi mara tatu na Ngao ya Jamii mara moja. Kurejea kwake Stamford Bridge leo ni tukio la kihistoria linaloleta kumbukumbu nyingi, huku dunia ya soka ikisubiri kuona kama “The Special One” ataandika ukurasa mwingine wa kukumbukwa.