Nasikia hata watani wao Yanga waliingilia dili la kumtaka kocha huyu raia wa Bulgaria. Maswali ni mengi. Kwanza kabisa hatuna mipango ya muda mrefu. Ina maana bila ya Simba kucheza na Gaborone United basi leo Pentev asingekuwa kocha wa Wekundu wa Msimbazi.
Ina maana kwamba bila ya Simba kucheza na Gaborone United, basi Yanga nao wasingemuona Pentev. Kwanini hatukumuona huyu kocha kabla ya mechi ya Gaborone United? Hapa ndio tunapogundua kwamba mpira wetu ni bora liende tu. Hatuna mipango ya muda mrefu.
Hatuandiki chini kinachopaswa kufanywa kwa msimu mzima. Kitu chochote kinaweza kutokea muda wowote. Hatuna mpango A wala B. Kila kitu kinaweza kutokea ghafla ghafla tu. Simulizi ya namna ambavyo kuna wachezaji wengi wamesajiliwa na timu hizi kwa sababu waliwahi kuzifunga. Basi. Sio kwamba walimchunguza mchezaji hapo awali, hapana! Ni kwa sababu amewafunga tu, lakini hakukuwa na uchunguzi yakinifu kuhusu mchezaji mwenyewe kabla ya pambano dhidi yake.
Ni hadithi ya Ditram Nchimbi pia. Aliwafunga Yanga mabao matatu na hapo hapo Yanga wakaanza kukimbizana na saini yake bila ya kujali kwamba mchezaji mwenyewe alikuwa hajawahi kufunga mabao zaidi ya kumi katika msimu mmoja. Alipotua Yanga mabosi ndio wakaanza kugundua upungufu mwingi kwake. Kama wangekuwa wamemchunguza awali si ajabu wasingemchukua kwa sababu tu alikuwa amewafunga mabao matatu katika mechi moja.
Kila la kheri kwa kocha mpya Msimbazi. Kitu kizuri kwa Simba ni kwamba wamemchukua mapema kabla ya msimu haujachanganya na atakuwa na muda mrefu wa kuwajua wachezaji wake kabla mambo hayajafika mbali.
— LEGEND, Edo Kumwembe [JichoLaMwewe]