DAR ES SALAAM:MWANAMITINDO na msanii maarufu wa Bongo Movie, Hamisa Mobetto, anatarajiwa kupamba usiku wa Tanzania Fashion Festival utakaofanyika Oktoba 18 katika ukumbi wa Delta Hotel, Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na SpotiLeo,Msemaji wa tamasha hilo, Bhoke Egina, amesema mwaka huu wameamua kuvunja mtindo wa zamani kwa kuwaleta wanamitindo wenye maumbo halisi ya Kiafrika.
“Kwa muda mrefu tasnia ya mitindo imekuwa ikihusishwa zaidi na wasichana warefu wembamba. Safari hii tumeamua kuonesha kuwa hata wanawake na wanaume wenye maumbo ya Kibantu wanaweza kuonekana vizuri katika mavazi ya kisasa,” amesema Bhoke.
Amefafanua kuwa jina la Hamisa Mobetto liliibuka kwa ajili ya kufungua tamasha hilo kutokana na muonekano wake wa Kiafrika, umaarufu wake, pamoja na mchango mkubwa alioutoa kwenye tasnia ya mitindo.
“Hamisa ana mvuto wa kipekee, umbo la Kibantu na huvaa mavazi ya mitindo kwa ufanisi mkubwa. Kwa sasa tunaweza kusema ameliteka soko la mitindo Tanzania,” ameongeza.
Bhoke alisema lengo kuu la tamasha hilo ni kutoa nafasi kwa wabunifu chipukizi pamoja na nguli wa mitindo kuonesha vipaji vyao, huku wakipinga dhana potofu kwamba mitindo ni ya watu wembamba pekee.
Mbali na Hamisa, wasanii wengine waliotajwa kushiriki ni pamoja na Jux, Phina na Nandy, ambao wote wamekuwa mstari wa mbele kuendeleza tasnia ya mitindo nchini.
Aidha, Bhoke ametoa wito kwa kampuni na taasisi mbalimbali kujitokeza kudhamini tamasha hilo, akisisitiza kuwa washiriki wa mitindo hawatalipia gharama yoyote, huku mapato ya viingilio yakitumika kugharamia maandalizi.
Viingilio vitakuwa kama ifuatavyo: Sh20,000 (kawaida), Sh60,000 (VIP) na Sh1,000,000 kwa meza ya watu 10 (VVIP).
The post Hamisa Mobetto kupamba Tanzania Fashion Festival first appeared on SpotiLEO.