SINGIDA:TIMU ya Singida Black Stars imeanza rasmi maandalizi kuelekea mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Flambeau du Centre kutoka Burundi, utakaochezwa Oktoba 19 mwaka huu.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi, Msemaji wa klabu hiyo, Hussein Masanza, alisema maandalizi hayo yanahusisha mazoezi ya kikosi kizima na michezo ya kirafiki ili kuimarisha hali ya wachezaji kabla ya safari.
“Tumeshanza maandalizi ya mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Flambeau du Centre. Timu itasafiri Oktoba 17, lakini kabla ya hapo tutacheza mechi kadhaa za kirafiki kwa ajili ya kujipima na kujiweka imara,” alisema Masanza.
Aliongeza kuwa lengo la michezo hiyo ya kirafiki ni kuhakikisha kikosi kinakuwa kwenye ubora wa juu kimwili na kiakili kabla ya safari ya kuelekea Burundi.
Singida Black Stars chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi, walisema dhamira yao ni kufanya vizuri hatua za awali na kutinga hatua ya makundi.
Mchezo wa awali, walitoka kuitoa Rayon Sports ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1. Mchezo wa kwanza walishinda ugenini 1-0 na ule wa nyumbani walishinda 2-1.
The post Singida Black Stars wajiwinda na Flambeau first appeared on SpotiLEO.