MADRID: UONGOZI wa LaLiga umethibitisha kuwa Mechi ya Ligi Kuu ya Hispania (LaLiga) kati ya Barcelona na Villarreal, iliyokuwa imepangwa kufanyika nchini Marekani, imefutwa rasmi kufuatia upinzani mkali ulioibuka nchini humo tangu kutangazwa kwa uamuzi huo.
Mchezo huo, uliopangwa kuchezwa Desemba 20 kwenye Uwanja wa Hard Rock, jijini Miami, ulikuwa uwe wa kwanza wa LaLiga kuchezwa nje ya Hispania na pia wa kwanza kwa ligi yoyote kubwa ya Ulaya kufanyika nje ya bara hilo.
Katika taarifa yake, LaLiga imesema:
“Baada ya mazungumzo na waandaaji wa mechi rasmi ya LaLiga huko Miami, wameamua kufuta mchezo huo kutokana na hali ya sintofahamu iliyojitokeza nchini Hispania katika wiki za hivi karibuni.”
“Tunasikitika sana juu ya uamuzi huu, kwani ulikuwa fursa ya kihistoria na ya kipekee kwa ajili ya kulifanya soka ya Hispania kuwa la kimataifa zaidi. Kuandaa mechi rasmi nje ya mipaka yetu kungekuwa hatua muhimu katika kukuza mashindano yetu duniani.”
Ingawa mpango huo ulikuwa umeidhinishwa na UEFA, bado ulikuwa unasubiri idhini ya mwisho kutoka FIFA. Wachezaji wa LaLiga waliendesha mgomo wa kimya wikiendi iliyopita kwa kusimama bila kusogea wakati wa kuanza kwa mechi, lakini maandamano hayo hayakuoneshwa kwenye matangazo rasmi ya televisheni badala yake, kamera zilionesha mabango yenye ujumbe: “Commitment to peace.”
LaLiga ilisisitiza kuwa mpango huo ulizingatia kanuni zote na kwamba mechi hiyo isingehatarisha usawa kwenye ushindani wa ndani wa Ligi.
The post Mechi ya Barcelona vs Villarreal Marekani yafutwa first appeared on SpotiLEO.