LONDON: MOJA ya changamoto chache zilizokuwa zikiiandama Arsenal msimu huu imekuwa ukame wa mabao kutoka kwa mshambuliaji wao wa bei ghali Viktor Gyokeres, lakini nyota huyo ameondoa mashaka hayo baada ya kurejea kwenye kiwango chake kwa kufunga mara mbili katika ushindi wao wa 4-0 dhidi ya Atletico Madrid usiku wa Jumanne.
Gyokeres, ambaye Arsenal ilimsajili kutoka Sporting kwa pauni milioni 64, alifunga bao la tatu na la nne kwa timu yake katika mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akisitisha ukame wa mechi tisa bila kufunga bao kwa klabu au timu ya taifa.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden alitabasamu alipokuwa akitolewa uwanjani mwishoni mwa mchezo, huku kocha Mikel Arteta akisema Gyokeres mwenye umri wa miaka 27 alistahili kabisa shangwe alizopata kutoka kwa mashabiki wa Arsenal.
“Nadhani alistahili, kwa sababu kila kitu tulichokuwa tukiona katika mchango wake kwa timu kilikuwa kikubwa alikuwa akisaidia sana katika maeneo mengi, isipokuwa kufunga mabao katika wiki chache zilizopita,”
“Haikuwa suala la mjadala. Ilikuwa ni kumtia moyo kuendelea kuamini uwezo wake, kujiweka katika hali ya utulivu na kucheza kwa uhuru. Ukiangalia wachezaji wenzake, kwenye picha na video, wote walifurahia sana kwa niaba yake.”
“Anatufanya tuwe timu bora zaidi. Nafikiri sasa tumekuwa vigumu kutabirika. Ana nguvu, anavyoshambulia mpira na kuumiliki, ni jambo la kipekee. Leo amefunga mabao mawili tofauti kabisa, na naamini hii ni mwanzo wa mfululizo mzuri wa mabao kwake.” – alisema Arteta mbele ya waandishi wa habari.
Bao la kwanza la Gyokeres lilitokana na shuti dhaifu lililopigwa na kuingia wavuni baada ya kuguswa na beki wa Atletico, huku bao la pili likitokana na mpira wa kona uliopigwa na Gabriel na kumpa nafasi Gyokeres kumalizia kwa urahisi.
Gyokeres sasa ana jumla ya mabao matano msimu huu, yakiwemo matatu katika Ligi Kuu ya England, na alionekana wazi kufurahia kurejea kwenye ubora wake wa kufumania nyavu.
The post Arteta atia neno kiwango cha Gyokeres first appeared on SpotiLEO.