Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtangaza Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Angel Gamondi kutoka Argentina, kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars. Uteuzi huu unakuja baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Hemed Suleiman “Morocco”, kuachana na TFF kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na TFF leo, Novemba 4, 2025, mazungumzo kati ya TFF na uongozi wa Singida Black Stars tayari yamekamilika, na Gamondi amekubali kuchukua majukumu hayo mapya.
Kocha huyo ambaye aliwahi pia kuinoa Young Africans SC (Yanga), anatarajiwa kuiongoza Taifa Stars kwenye michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba mwaka huu.






