DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Yanga Clement Mzize amefanyiwa upasuaji wa goti utakaomweka nje wiki 8 hadi 10 ambayo ni sawa na miezi miwili mpaka mitatu.
Mzize aliumia kwenye mchezo wa awali dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola, wakati Yanga ikiichapa timu hiyo mabao 3-0 na baadaye akajitonesha jeraha hilo akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga Ally Kamwe, baada ya ushauri wa jopo la madaktari wa klabu, kwa kushirikiana na benchi la ufundi na mchezaji mwenyewe, imekubaliwa kwamba Mzize afanyiwe upasuaji maalum ili kutatua tatizo hilo kikamilifu.
“Mara ya mwisho tuliwajulisha kuhusu hali ya majeraha ya mchezaji Clement Mzize. Baada ya ushauri wa jopo la madaktari wakishirikiana na benchi la ufundi na mchezaji mwenyewe tulikubaliana afanyiwe upasuaji,”amesema.
Alisema: “Maamuzi haya yalikuja baada ya kuona anaendelea kupata maumivu kwenye goti lake kila alipokuwa akirejea uwanjani. Nipende kuutangazia umma kuwa, mchezaji Clement Mzize atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nane mpaka kumi,” alisema Kamwe.
Hivyo, mchezaji huyo anatarajiwa kukosa michezo kadhaa ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ile yah atua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
The post Mzize kukaa nje wiki 8–10 first appeared on SpotiLEO.




