LOS ANGELES: MSANII maarufu wa muziki wa hip-hop, Asap Rocky, amefunguka kuhusu furaha yake kubwa ya kuwa baba wa mtoto wa kike kwa mara ya kwanza, akisema maisha yake sasa yamejaa upendo na mwanga zaidi.
Rocky, mwenye umri wa miaka 37, na mpenzi wake Rihanna, walimkaribisha mtoto wao wa tatu, Rocki Irish Mayers, mwezi Septemba mwaka huu.
Akizungumza na Extra, rapa huyo alisema kwa furaha: “Kuwa baba wa msichana ni kitu cha ajabu kabisa. Hebu niangalie, ninafuraha kweli!”
Rocky na Rihanna tayari wana watoto wa kiume wawili RZA (miaka 3) na Riot (miaka 2) na sasa wamebarikiwa na mtoto wa kike ambaye amezidi kuifanya familia yao kuwa na furaha zaidi.
Chanzo cha karibu na familia hiyo kiliiambia jarida la People kwamba wawili hao walikuwa na mpango wa kupata watoto ambao wako karibu kwa umri tangu awali.
“Rihanna amekuwa akitamani familia kubwa. Wote wawili wana furaha kubwa kuona familia yao ikikua. Walitaka watoto wao wakue pamoja na kuwa na uhusiano wa karibu,” kilisema chanzo hicho.
Mbali na maisha ya kifamilia, Asap Rocky pia amepokea heshima kubwa baada ya kutunukiwa tuzo ya mwanamitindo ‘Fashion Icon Award’ katika tuzo za CFDA Fashion Awards 2025.
Kwa upande wa Rihanna, nyota huyo wa muziki na urembo ameweka kipaumbele chake kwenye malezi ya watoto kuliko kitu kingine chochote.
Chanzo kingine kiliiambia People kuwa sasa “Rihanna ni mama wa mfano”.
“Anawachukua watoto kila anapokwenda, hata kwenye safari za kikazi. Hachoki wala halalamiki, anafurahia maisha. Anaonekana mwenye furaha kuliko wakati wowote.”
Asap Rocky naye anaelezwa kuwa mwenye msaada mkubwa kwa Rihanna tangu walipoanza maisha ya wazazi.
“Wanafanya kazi nzuri sana katika kulea watoto wao,” alisema mtu wa karibu na wanandoa hao. “Rocky ni mchapakazi na mwelewa, na Rihanna anaonekana kuwa na furaha ya kweli.”
Kwa sasa, Rihanna na Asap wanaendelea kufurahia maisha ya familia yao changa, wakijivunia watoto watatu na mafanikio makubwa katika muziki, mitindo, na biashara huku wakionesha kwamba upendo na umoja ndiyo mitindo bora kuliko yote.
The post Asap Rocky:Kuwa Baba wa wasichana ni kitu cha Ajabu! first appeared on SpotiLEO.



