THAILAND: SHEREHE ya Miss Universe 2025 iliyofanyika nchini Thailand iligeuka kuwa vurugu kubwa baada ya Mkurugenzi wa Taifa wa Shindano hilo, Nawat Itsaragrisil, kufanya tukio lililodaiwa kuwa ni udhalilishaji kwa mshiriki kutoka Mexico, Fátima Bosch, kitendo kilichosababisha washiriki zaidi ya 20 kuamua kutoka ukumbini kwa pamoja kwa ishara ya kupinga tukio hilo.
Tukio hilo lilitokea wakati wa matangazo ya moja kwa moja mtandaoni, ambapo Nawat anayejulikana kwa mtindo wake mkali wa uongozi alimshutumu Bosch kwa kutofuata maagizo ya wadhamini, hasa kuhusu kutotangaza vya kutosha utalii wa Thailand kupitia mitandao yake ya kijamii.
Hali ilizidi kuwa mbaya pale Nawat alipomuita Bosch mpumbavu na kuagiza walinzi wamtoe nje ya ukumbi, baada ya mrembo huyo kujaribu kujitetea.
Video ya tukio hilo ilisambaa kwa kasi mitandaoni, na kusababisha hasira kubwa miongoni mwa mashabiki na washiriki wa mashindano hayo duniani kote.
Nje ya ukumbi, Bosch alizungumza na waandishi wa habari kwa utulivu na ujasiri, akisema:
“Nataka nchi yangu ijue kuwa sioni aibu kusema ukweli wangu. Ninataka kuona heshima na uwezeshaji zaidi kwa wanawake katika mashindano haya.”
Kauli hiyo iliibua wimbi la mshikamano kutoka kwa washiriki wengine, wakiwemo Miss Universe anayetetea taji, Victoria Kjær Theilvig wa Denmark, ambao wote waliondoka kwa pamoja kama ishara ya kupinga unyanyasaji na ubaguzi wa kijinsia.
Mitandao ya kijamii ililipuka kwa jumbe za kumuunga mkono Bosch, ambapo maelfu ya watu walimsifu kwa ujasiri wake na kulaani utamaduni wa unyanyasaji na hofu unaodaiwa kuenea katika tasnia ya urembo.
Baada ya shinikizo kuongezeka, Nawat alilazimika kuomba radhi hadharani kupitia matangazo ya moja kwa moja, akidai maneno yake yalieleweka vibaya na akionesha majuto kwa kuumiza hisia za wengi. Hata hivyo, ombi lake la radhi halikupunguza hasira za umma.
Rais na mmiliki mwenza wa Shirika la Miss Universe, Raúl Rocha, alilaani vikali tukio hilo, akisema matendo ya Nawat yalikuwa ya kudhalilisha na kukosa heshima.
“Sitakubali maadili ya heshima na utu wa wanawake yavunjwe,” alisema Rocha kwa msisitizo.
Rocha alitangaza kuwa viongozi wakuu wa Miss Universe wataelekea Thailand kurejesha utulivu, akiwemo Afisa Mtendaji Mkuu mpya wa Miss Universe, Mario Búcaro kutoka Guatemala, na Ronald Day, Mkurugenzi Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa shirika hilo.
Kwa sasa, tasnia ya urembo duniani imegubikwa na mjadala mkubwa kuhusu heshima, mamlaka, na nafasi ya wanawake, huku tukio la Thailand likionekana kama alama ya mabadiliko yanayohitajika ndani ya mashindano hayo ya kimataifa.
The post Taharuki yazuka Shindano la Miss Universe 2025 first appeared on SpotiLEO.



